Search in This Blog

SALHA WA HAMMER Q AFUKUZWA KAZI …KISA KUIMBA NA MUMEWE, BOSI WAKE ALIWAHI KUMKATAZA ASIOLEWE

MWIMBAJI nyota wa Dar Modern Taarab, Salha Abdallah ambaye ni mke wa Hammer Q amefukuzwa kazi kundini humo.

Kutimuliwa kwa Salha kunaonyesha kuwa hali si shwari ndani ya Dar Modern Taarab baada ya wiki chache zilizopita kiongozi wa kundi hilo Mridu Ally kutangaza kujiengua.

Salha amefukuzwa baada ya kushiriki kuimba wimbo nje ya kundi.

Kwamba Salha kwa kushirikiana na mumewe (Hammer Q) wamerekodi wimbo wao binafsi uliopewa jina la “Wapendanao”.

Wimbo huo uliingia kwenye vituo vya radio mwishoni mwa wiki iliyopita na sasa wawili hao wako kwenye hatua za kutengeneza video.

Salha amesema kuwa alifukuzwa Jumatatu (juzi) kwa kupitia ujumbe wa simu ya mkononi.

“Mmililki wa bendi (Feresh Abdallah) alintumia meseji kupitia simu yangu na kuniambia nakala ya ujumbe huo imekwenda kwa wasanii wote sambamba na baba yangu mzazi,” alisema Salha.

Salha anaeleza zaidi: “Kwa hali iliyo Dar Modern ni wazi kuwa sikutendewa haki, Hammer Q ni mume wangu sidhan kama kulikuwa na ubaya kuimba nae pamoja.

“Wako wasanii wengi Dar Modern wanafanya kazi za nje (Ndondo) kwenye bendi zingine na uongozi unajua lakini hawajawahi kuchukuliwa hatua yoyote.

“Hili ni kundi ambalo nililitumikia kwa moyo wangu wote sikuwahi kufikiria kuhama, vikundi vingi vimewahi kunihitaji lakini sikuthubutu kuondoka.

“Niliuheshimu mkataba wangu, hata Five Stars iliposukwa upya walinifuata na kunipa pesa ili nijiunge nao lakini nikachomoa.

“Fereshi alipaswa kuthamini utu niliouonyesha kwenye bendi yake, sijawahi kulipwa malipo ya ushiriki wa albam lakini sikuthubutu kuonyesha utovu wa nidhamu.”

Salha anadai anapata shaka kuwa pengine kuna ajenda ya siri ndani uamuzi huo.

“Tangu nimeolewa maisha yangu ndani ya Dar Modern yamekuwa yakizungukwa na kisirani kutoka kwa boss.

“Aliwahi kukataza waimbaji wa kike wasiolewe, hata ndoa yangu hakuifurahia, sielewi ni kwanini.

“Kabla sijaolewa niliimba wimbo mmoja na AT lakini sijakutana na hatua kama hii wala kupewa onyo lolote’” alisema Salha anayetamba na wimbo “Nauvua Ushoga”.

Salha ambaye amedumu Dar Modern tangu mwaka 2005 amesema kwa sasa anajipanga kumalizia albam ya pamoja na mumewe na iwapo itatokea bendi ambayo atakubaliana nayo mambo ya msingi basi atajiunga nayo.

Uchunguzi  umebaini kuwa miongoni wasanii wa Dar Modern wanaopiga ‘ndodo’ (kazi za nje) ni  mwimbaji Twaha Mohamed ambaye kwa muda mrefu amekuwa akilitumikia kundi la Mapacha Watatu.

Licha ya Twaha kutambulishwa Mapacha Watatu mbele ya vyombo vya habari wakati wa uzinduzi wa albam ya “Yarabi Nafsi” Twaha bado pia anaendelea kuitumikia Dar Modern.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger