Dar es Salaam. Wakati Simba ikiendelea kusotea pesa za kuuzwa Emmanuel
Okwi klabu ya Etoile du Saleh ya Tunisia, klabu hiyo imesema mpango wake
wa kumpiga bei kiungo, Amri Kiemba kwenda Raja Casablanca ya Morocco
utatimia iwapo klabu hiyo itakubali kutoa siyo chini ya Sh500 milioni.
Raja
Casablanca imepiga hodi Msimbazi kutaka kumsajili Kiemba baada ya
kuvutiwa naye wakati walipomwona akiichezea Timu ya Taifa (Taifa Stars)
dhidi ya Morocco zaidi ya wiki moja iliyopita.
Akizungumza na
Mwanannchi jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya usajili ya
Simba Zakaria Hanspope alisema, kiwango hicho cha fedha ndiyo thamani
ya sasa ya Kiemba.
“Tayari tumezungumza na Raja Casablanca na
kweli wameonyesha nia ya kumtaka Kiemba, lakini kwetu hakuna namna
yoyote ya kumtoa bila Sh500 milioni kuwekwa mezani,” alisema Hanspope.
“Nilipokwenda
kwao (Morocco) Rais wa klabu alikuwa Uturuki, tunasubiri arejee ili
tuwatumie mchanganuo mzima wa mauzo ya Kiemba,” alisema.
Hanspope,
alisema angependa kuona klabu yake inafanya biashara ya kuwauza
wachezaji kwa faida. Tunatakiwa kuwalipa makocha, kuingia mikataba na
wachezaji, mambo yote haya yanahitaji pesa. Hatuwezi tena kufanya
biashara isiyo na faida kwa upande wetu,” alisema zaidi bosi huyo.