RAIS Barack Obama leo anaanza ziara ya
siku mbili nchini akitokea Afrika Kusini ikiwa ni sehemu ya ziara yake
ya kuzuru Bara la Afrika.
Safari ya Obama ilianza Juni 26 nchini
Senegal, kisha akaenda Afrika Kusini na anakuwa Rais wa tatu wa Marekani
kuzuru Tanzania akiwa madarakani.
Wengine ambao walipata kufanya hivyo ni
Rais Bill Clinton na George W. Bush ambao walifika nchini kwa nyakati
tofauti wakiwa madarakani.
Katika ziara hiyo, Obama anafuatana na mkewe, Michelle na mabinti zao Sasha na Malia.
Sababu ya ziara
Akizungumzia ujio wa kiongozi huyo wa
taifa kubwa duniani, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt alitaja
sababu zilizomsukuma Rais Obama kuja kuwa ni kutokana na Tanzania kuwa
mfano wa nchi zenye utawala bora na ustawi wa demokrasia.
Nyingine ni juhudi zinazofanywa na
Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo kwa mujibu wa
Balozi huyo yanaivutia Serikali ya Marekani kwani yatachangia katika
kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Eneo lingine ni kusaidia ukuaji na
uendelezaji wa viongozi vijana. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo
baadhi ya vijana wake wamekuwa wanapata mafunzo ya uongozi chini ya
mpango uliozinduliwa na Rais Obama mwaka 2010.
Obama alianzisha programu ya kuandaa
viongozi wa kizazi kijacho “Rais Obama anataka kusaidia kuandaa viongozi
wa kizazi kijacho kwa Afrika kusimamia vizuri rasilimali za bara hili.”
Na kwa kinywa chake juzi alisisitiza
alipozungumza na vijana Soweto, Afrika Kusini. Lakini pia katika ziara
hiyo, atataka kusikia na kujionea baadhi ya miradi ambayo inafadhiliwa
na Serikali yake.
Tanzania ni kati ya nchi zinazoongoza
kwa kupokea fedha nyingi za misaada ambazo zinafikia dola milioni 750.
Eneo lingine ni suala la chakula ambapo Balozi alisema Marekani inaunga
mkono jitihada za Serikali kujitosheleza kwa chakula na inafadhili
mkakati wa kukuza kilimo Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Mpango huo unafadhiliwa na Mfuko wa Rais
wa Marekani ujulikanao kama ‘Feed the Future’ wenye lengo la kuifanya
Tanzania kupiga hatua katika kilimo.
Ratiba
Atakapowasili katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere na ndege yake Air Force One, atazindua
barabara mpya upande wa Mashariki wa lango la kuingia Ikulu ambayo
inatarajiwa kuitwa Barack Obama.
Baada ya shughuli hiyo atazungumza kwa
nyakati tofauti na wafanyabiashara wa nchi za Afrika na Marekani kwenye
Hoteli ya Hyatt Regency, Dar es Salaam. Amepanga pia kuzungumza na
maofisa wa Ubalozi wa Marekani nchini.
Baadaye atahudhuria dhifa ya taifa usiku ambayo imeandaliwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete, Ikulu, Dar es Salaam.
Kesho ataweka shada la maua sehemu
ulipokuwa Ubalozi wa Marekani ikiwa ni kumbukumbu ya watu waliouawa
katika shambulizi la kigaidi la bomu mwaka 1998, Dar es Salaam.
Pia atatembelea mitambo ya kufua umeme
ya Kampuni ya Symbion iliyoko Ubungo. Rais Obama atatoa hotuba
kuzungumzia mikakati ya Marekani ya kusaidia Afrika kuzalisha nishati ya
umeme.
Michelle atakuwa na ratiba yake ambapo
leo atapata staftahi na mwenyeji wake, Salma Kikwete katika ofisi za
Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (Wama), Dar es Salaam.
Pia atatembelea sehemu ulikokuwa ubalozi
wa Marekani na kisha atashuhudia onesho la utamaduni la kikundi cha
Baba wa Watoto, ambacho kinajumuisha watoto wa mitaani wenye umri wa
kuanzia miaka mitano hadi 18 kwenye Makumbusho ya Taifa.
Kesho Michelle atahudhuria mkutano na
wake wa marais wa nchi za Afrika ambao pia utahudhuriwa na mke wa Rais
wa zamani wa Marekani, George Bush, Laura.
Barabara kufungwa
Wakati akiwa nchini kutokana na ulinzi
kuwa mkubwa ni wazi kuwa mitambo ya mawasiliano wanayotumia inaweza pia
kuathiri upatikanaji wa mawasiliano ya simu za mkononi. Hali hiyo ni
wazi kuwa itazusha adha kubwa kwa watumiaji wa simu za mkononi.
Lakini pia hali ya usafiri wa umma
utakuwa wa adha kubwa kutokana na ugeni huo kutumia baadhi ya barabara
muhimu za Jiji la Dar es Salaam. Hivyo inashauriwa kuwa wafanyakazi
ambao watakaokwenda kazini wadamke alfajiri ili kuepuka adha hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar
es Salaam jana kwenye ukumbi wa Majadiliano ya Pamoja kwa Manufaa ya
Wote, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, aliwaomba radhi
wananchi kwenye barabara ambazo msafara huo utapita kwa usumbufu
watakaopata kwa muda. Msafara huo utapita barabara za Nyerere, Gerezani,
Sokoine Drive hadi Ikulu kwa kupitia lango la Mashariki.
Licha ya barabara hizo kufungwa, waenda
kwa miguu ni ruksa kupita pembeni mwa barabara hizo isipokuwa magari,
maguta, bajaji, pikipiki na baiskeli hazitaruhusiwa kupita au kukatiza.
Barabara ya Nyerere itafungwa leo
kuanzia saa 6.30 mchana hadi saa 9.30 alasiri na kesho kuanzia saa 3
asubuhi hadi saa 5 asubuhi, zitafungwa barabara za Ali Hassan Mwinyi,
Sam Nujoma na Morogoro na Nelson Mandela ambayo ataitumia wakati akienda
uwanja wa ndege kurejea Marekani.
Wananchi wote na hasa wanaofanya
shughuli za kiuchumi katika maeneo ambayo msafara utapita, wanatakiwa
kujipanga pembeni mwa barabara na maeneo ambayo vikundi vya ngoma,
burudani na tarumbeta vitakuwa vimejipanga kuanzia eneo la njiapanda ya
Kipawa, Jet Club, Vingunguti, Tazara, Kamata, Relwe Gerezani na Posta ya
zamani eneo la Azania Front kumlaki mgeni huyo.
Julai 2, Rais Obama atatembelea mitambo
ya kufua umeme ya Symbion Ubungo saa 4 asubuhi na kisha msafara wake
utapita Nelson Mandela, Tazara hadi uwanja wa ndege na kuondoka saa 5.20
asubuhi.
Neema kwa vijana
Obama ametangaza mpango wa kuwajengea
uwezo viongozi vijana wa Afrika kwa kuwapa mafunzo ya uongozi katika
vyuo vikuu vya Marekani hasa katika masuala ya utawala, biashara na
uongozi.
Katika hotuba yake katika Chuo Kikuu cha
Johannesburg juzi jioni, alisema hatma ya Afrika iko mikononi mwa
vijana; hivyo ni lazima wawezeshwe ili kuliongoza vizuri bara hili.