NAIBU wa Rais Bw William Ruto, jana
alivunja kimya chake kuhusu hatua ya rais wa Marekani Barack Obama
kutozuru humu nchini kwa kusema hatua hiyo haina madhara yoyote kwa
Kenya.
Huku akiongea
katika kanisa la Katoliki la St Gabriel Bahati, kaunti ya Nakuru, Bw
Ruto alisema nchi hii ina 'marafiki’ wengine wengi duniani ambao inaweza
kushirikiana nao huku akiongezea kuwa hatua ya rais Obama kukwepa
kutembelea Kenya haiwezi kutatiza kwa vyovyote vile uhusiano mwema
uliopo wa kibiashara baina ya Marekani na Kenya.
“Tunaiheshimu nchi ya Marekani nayo inafaa kuwaheshimu Wakenya,” akasema Bw Ruto.
Alisema
serikali tayari imeanzisha mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa
kibiashara na mataifa mengine huku akikariri kuwa safari ya Rais
Uhuru Kenyatta nchini Uganda ambapo alikutana na rais wa nchi hiyo
Yoweri Museveni na mwenzao wa Rwanda rais Paul Kagame kujadili jinsi
nchi hizo tatu zinaweza kushirikiana kibiashara, ni miongoni mwa
mikakati hiyo.
“Nchi yetu inamcha
Mungu na kamwe hatutaruhusu mataifa ya kigeni kutuletea tamaduni ambazo
zinakinzana na desturi zetu,” akasema Bw Ruto huku akirejelea hotuba ya
Rais Obama nchini Senegal ambapo aliitaka nchi hiyo kuheshimu haki za
Mashoga.
Rais Obama
ambaye yuko barani Afrika alikosa kutembelea Kenya na badala yake
akazuru mataifa ya Senegal, Afrika Kusini na Tanzania; kwa kile
alichokitaja kuwa haukuwa wakati mwafaka wa kutembelea nchi hii kwani
viongozi wake wanakumbwa na mashtaka katika mahakama ya Kimataifa ya
kupambana na uharifu wa Kibinadamu (ICC) japo aliahidi kuitembelea Kenya
kabla ya kipindi chake kama rais wa Marekani.