Hii mada nimeona niiandike haraka sana
kwani tunakoelekea kubaya wanawake wenzangu, siku hizi eti wanawake
ndiyo tunaongoza kufumaniwa aibu sana hii, tunaziaibisha familia zetu na
tulikotoka jamani.
Hivi ni kwa sababu gani wanawake
tumekosa haya na kuamua kushindana na wanaume, wakati mwingine ni hulka
tu ya mtu, kwa nini usiache tabia zako huko kwenye ujana unataka
uziingize mpaka kwenye ndoa, hivi mnajua maana ya ndoa lakini? Wenye
tabia mbaya waseme kufumaniwa sasa basi.
Sasa niwaambie basi si wanaume wote
wakiwa hawapo nyumbani wameenda kujiachia na wanawake wengine la hasha,
mwanamke jiheshimu kulingana na heshima yako, mwanaume wako anavyotoka
nje ya nyumba au mji anakuwa amekwenda kutafuta kwa ajili yenu.
Jaribu kumuonea huruma
Kwa mwanamke mwenye mapenzi na mumewe
anatakiwa kumuonea huruma mume wake hasa pale anapogundua amekwenda
kufanya kazi kwa ajili ya kutafuta riziki ya familia, kwani anachotafuta
ni kwa ajili familia nzima.
Mashosti, baadhi ya wanawake wana tabia
mbaya, wamekuwa ni watu wa kuingiza wanaume ndani ya nyumba zao ambazo
wanaishi na waume wao wa ndoa, hivi hujisikii vibaya kuingiza jasho la
mwanaume mwingine kwa mume wako wa ndoa? Kwa nini unamuadhibu hivyo,
amekosea nini?
Wengi wanaofanya hivyo ni wale ambao waume zao wanasafiri kwenda nje ya mji!
Mwanamke mwenzangu ni kwa nini uwe na
fikra mbaya kuwa mumeo lazima kila mkoa ana mke na wewe unaamua
kujiingiza pabaya? Huoni kufanya hivyo ni kuamua kuleta magonjwa ndani
ya nyumba. Chunguzeni wanawake wengi siku hizi ndiyo sababu ya kuenea
ugonjwa wa Ukimwi lakini wanaume zao hawajui ni mbaya sana mashosti
tunatakiwa kubadilika, hali imekuwa mbaya.
Kama unahisi mumeo ana mtu fanya hivi
Kama unahisi mumeo ana mwanamke kwa
hisia tu, mchunguze na ukigundua ni kweli mketishe aache tabia hiyo
lakini nawe jishughulishe na ujasiriamali kwanza, kwa kujichanganya na
watu utasahau fikra potofu na utaweza kujiingizia kipato na siku
zitaenda utashtukia mnakaa vyema na mumeo, kama alikuwa kiruka njia
anarudi nyumbani.
Kwa kufanya hivyo familia yenu itakuwa yenye furaha na amani na kipato kitaongezeka kwa sababu wote mtakuwa mnajishugulisha.
Mume akisafiri fanya haya
Siku ya kusafiri mumeo hakikisha unakaa
naye chini kwa lugha ya upendo, unamuomba awe mwaminifu aendako kisha
unamuombea dua asafiri salama kwani huko atakutana na mengi.
Kuna ajali za barabarani na misukosuko
yote unayoijua kwa safari, sasa kwa dua na mashetani yanayopita yatapita
mbali kabisa hata kama anawaza kukusaliti atashindwa kwani akikumbuka
jinsi mlivyoagana roho itamsuta.
Jenga tabia ya kumuuliza amefika wapi na kumtakia safari njema awapo njiani.
Akikaribia kurejea nyumbani ufanye nini?
Siku ukiona mumeo anakaribia kurudi
hakikisha unafanya usafi wa mwili wako pasipo kawaida kama hupendezi
basi pendeza kwa ajili ya kumpokea mume, muandalie chakula kizuri na
uhakikishe unampikia kile roho inapenda.
Kabla ya kufunga mada hii nasisitiza
wanawake wenzangu ni aibu sana kufumaniwa acheni mambo ya mafiga matatu
ni mabaya na mwisho hayana faida yoyote kwani utapata aibu na ugonjwa
je, familia utamuachia nani? Wanawake wenzangu kwa leo niishie hapa
tukutane kwenye mada nyingine wiki ijayo, Inshallah.