Search in This Blog

MBEGU, MAYAI YA UZAZI ZAGEUZWA BIASHARA NCHINI


Kadri matatizo ya uzazi yanavyoendelea kukithiri duniani kote, wataalamu wa afya nao wanaendelea kuvumbua njia mbalimbali za kuwasaidia wenye matatizo ya kukosa watoto.
Katika harakati hizo Kliniki ya Upandikizaji ya Dar es Salaam, (Dar IVF and fertility clinic) wameanzisha huduma ya kununua mbegu za kiume na mayai ya wanawake, kwa ajili ya kutoa huduma ya uzazi kwa njia ya upandikizaji au IVF.
Gazeti hili lilipiga simu katika kliniki hiyo kutaka kujua iwapo linaweza kuchangia mayai na daktari aliyekuwapo zamu alijibu; “inawezekana”.
Daktari huyo ambaye hata hivyo alisema kliniki hiyo bado haijaruhusiwa kujitangaza katika vyombo vya habari, alisema kwa sasa kifaa cha kuhifadhi mayai (ya mwanamke) hakipo ila kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume kipo na wanapokea wachangiaji wanaotaka kuuza mayai hayo kwa makubaliano rasmi.
“Ukija tutajadiliana bei, kwa sasa hatuna bei rasmi, lakini nadhani ukija tutakubaliana. Siku ukiwa tayari njoo tujadili. Bei ni makubaliano,” alisema daktari huyo.
Alisema kwa kuwa kifaa cha kuhifadhi mayai hakipo hivyo mchangiaji atakapochangia mayai, yatatakiwa yatumike siku hiyo hiyo katika upandikizaji, lakini kifaa cha kuhifadhi mbegu za kiume, kipo.
Dk huyo (tunamuhifadhi jina kwa sababu ya sheria za hospitali hiyo), alisema mchangiaji wa mbegu au mayai atatakiwa kupimwa kwa kina, kwanza atapimwa damu kama ana maambukizi ya VVU, atapimwa iwapo ana maradhi ya urithi na kundi la damu kabla ya kukubaliwa kuchangia.
Tovuti ya kliniki hiyo inaeleza wazi huduma zinazotolewa ambapo mbali na uchangiaji wa mbegu na mayai, lakini huduma kuu ni kuwasaidia wenye matatizo ya uzazi, kupata watoto kwa njia ya upandikizaji.
Huduma nyingine ni kutibu matatizo ya ugumba kwa wanawake na wanaume, kuchagua jinsia ya mtoto, upasuaji wa kukaza kizazi kuzuia mimba kutoka (shridkar shuture) pamoja na huduma za matenite.
Madhumuni ya watu kuchangia mbegu au mayai ni katika kuhakikisha hakuna upungufu wa mbegu, na kuwasaidia wale wote ambao wameshindwa kutimiza ndoto za kuwa na familia.
Dk Henry Mwakyoma, Daktari Bingwa wa masuala ya uzazi wa Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili anasema, maendeleo hayo yanafanikiwa zaidi nchi za nje ambako kuna teknolojia na utayari wa watu.
“Kwa hapa kwetu kwanza teknolojia hii bado haijapata umaarufu, lakini ni lazima kuhakikisha kuwa Watanzania wenyewe wapo tayari kukubali uzazi wa njia hii,” alisema Dk Mwakyoma.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger