MTOTO wa kike mwenye umri wa miaka mitatu, Maryment Ibrahim ambaye 
anaishi Tandale jijini Dar es Salaam, hivi karibuni alipatwa na masahibu
 makubwa baada ya kutekwa nyara na kutoroshwa hadi Gairo mkoani Morogoro
 huku mtekaji akidaiwa kutaka apewe shilingi milioni 6 ili amuachie.
Tukio hilo la kusikitisha lilitokea Oktoba 16 mwaka huu baada ya 
kijana mmoja, anayefanya biashara ya kuuza chipsi anayejulikana kwa jina
 la Issa Ramadhani, kudaiwa kumchukua mtoto huyo aliyekuwa akicheza 
nyumbani kwao na kutoweka naye kabla ya wazazi wake kubaini na kwenda 
kutoa taarifa kituo cha Polisi Kijitonyama ‘Mabatini’.
Awali, ilidaiwa Ramadhan alikuwa na tabia ya kuwachukua watoto wadogo
 wa mtaani hapo na kuondoka nao na kuwarudisha baadaye, kitu 
kilichowafanya wazazi wa mtoto huyo kutokuwa na wasiwasi.
Wakizungumza na mwandishi wetu, wazazi wa mtoto huyo walisema 
waliamua kutoa taarifa polisi na kufunguliwa jalada nambari 
KJM/RB/8994/13 baada ya kupashwa kuwa mtekaji ambaye alishaacha kazi 
yake ya kukaanga chipsi, aliondoka muda mrefu na binti yao na hakukuwa 
na dalili za kurejea.
Baada ya kuhangaika kwa muda mrefu, wazazi hao pamoja na majirani 
walifanya uchunguzi wa chinichini na kufanikiwa kupata namba ya simu ya 
mtekaji huyo, lakini walifanikiwa kubadilishana naye ujumbe mfupi wa 
simu kwani hakuwa akipokea simu yake ya kiganjani.
Inadaiwa kuwa katika mawasiliano hayo, mtekaji alikataa katakata ombi
 la kumtaka amrudishe mtoto wao na kutaka apewe kiasi cha shilingi 
milioni 6 ili kutekeleza jambo hilo ingawa baadaye ilibainika jamaa huyo
 alikuwa Gairo mkoani Morogoro.
Wazazi hao walisema kuwa Oktoba 19 mwaka huu mmoja wa majirani 
walioguswa na tukio hilo aliyejitambulisha kwa jina la Justin Henry 
alijitolea kusafiri mpaka Gairo kumsaka mtoto na mtekaji wake jambo 
ambalo lilifanikiwa kwa kumpata mtoto akiwa mzima wa afya japokuwa 
mtekaji alishtukia na kukimbia.



