MKALI wa songi linalotamba runingani na redioni ndani na nje ya Bongo
la Number One, Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ amefunguka na
kuanika siri tano za kurudiana na Wema Isaac Sepetu ‘Madam’.
Wiki
mbili zilizopita, wakiwa Hong Kong, China, vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii viliripoti kurudiana kwa Diamond na Wema
waliomwagana takriban mwaka mmoja uliopita ambapo staa huyo wa Bongo
Fleva aliibuka na kukanusha vikali akidai kuwa picha zinazomwonesha yuko
na Wema ni za Filamu ya Temptations.
Akizungumza na Risasi Jumamosi kwa dakika ishirini katika mahojiano
maalum jijini Dar mara tu baada ya kutua kutoka China Jumatano
iliyopita, Diamond alikiri kufaidi penzi la Miss Tanzania huyo wa mwaka
2006.
Diamond alisema kuwa, Wema ndiye aliyetangulia kwenda China ambapo
yeye aliungana naye siku kadhaa baadaye akitokea kwenye shoo nchini
Malaysia.
SIRI YA KWANZA
Akianika siri za
kujikuta mikononi mwa mwigizaji huyo mwenye mashabiki wengi zaidi katika
tasnia ya filamu za Kibongo, Diamond alisema kwanza ni ukarimu aliopewa
na mrembo huyo.
Alisema kuwa alipotua Hong Kong alishangaa kukutana na mapokezi ya Wema kwenye uwanja wa ndege jambo ambalo hakulitegemea.
“Alinionesha ukarimu wa hali ya juu mno. Wakati tulipokuwa hapa Bongo tulikuwa hatusalimiani.
“Kuna vitu vingi vya ajabu vilitokea huko nyuma kati yangu na Wema.
Sikufikiria wala kuwaza kama anaweza akawa mkarimu kwangu kiasi kile.
Akaongeza: “Kwa mazingira yalivyokuwa, kwa namna yoyote lazima
mwanaume aliyekamilika arudishe moyo nyuma na kuacha mambo mengine
yaendelee.
“Kiukweli nisema tu kuwa hata tungekutana Morogoro au Dodoma kwa ukarimu ule mwisho wa siku tungerudisha uhusiano wetu.” SIRI YA PILI
Diamond alisema baada ya mapokezi ya nguvu, Wema alimpeleka kwenye
hoteli ya nyota tano (five stars) ambapo huko alipatiwa huduma ‘klasiki’
na kujiona kama yupo kwa mama Nasibu vile.
SIRI YA TATU
Alifunguka kuwa kitendo cha Wema kuwa mwenyeji wake China ambako
alikuwa mgeni hadi akapazoea nacho ni siri nyingine iliyochangia wao
‘kukumbushiana’.
SIRI YA NNE
Alisema kuwa
mwanadada huyo alimuonesha mapenzi mazito (yaani kutekwa kimapenzi)
hivyo haikuwa rahisi kumchomolea kwani waliishi kama ndiyo penzi jipya
linachipuka, akajikuta akiogelea naye.
SIRI YA TANO
Diamond alisema kuwa bado ana ndoto ya kupata mtoto kupitia kwa Wema
ambaye anajua kuwa alishamwambia lengo lake juu ya kupata naye uzao
hivyo katika nyakati za kukutana kwao anaamini ndoto itatimia.
HAKUNA CHA FILAMU
Alipoulizwa juu ya madai kuwa walikuwa wakirekodi filamu, Diamond
alifunguka kuwa hakuna cha filamu wala sinema na kama kuna mtu anasubiri
filamu atakaa sana.
“Naomba nikiri kuwa kweli zile picha hazikuwa za filamu wala nini
bali ndivyo hali halisi ilivyokuwa kati yangu na Wema kule China.
“Pia naomba niseme kuwa uhusiano wetu wa kimapenzi uliishia China na
sasa hivi tumebaki kama kaka na dada na ni ruksa kila mtu kumtumia
mwenzie katika kazi mbalimbali kama ataona kuna ulazima wa kufanyika
hivyo,” alisema Diamond.
Hii ni mara ya kwanza kwa Diamond au Sukari
ya Warembo kukiri kuwa kweli alirudisha penzi lake kwa Wema walipokuwa
nchini humo wakijiachia.
PENNY HANA CHAKE?
Kwa mujibu wa watu wa karibu wa Diamond, ukifuatisha simulizi hiyo ya
mapenzi kati ya msanii huyo na Wema, ni dhahiri kuwa mpenzi wa sasa wa
jamaa huyo, Penniel Mungilwa ‘VJ Penny’ hana chake kufuatia usaliti huo.
Hata hivyo, jitihada za kumtafuta Penny ziligonga mwamba kufuatia
simu yake kuita bila kupokelewa lakini juzi wanahabari wetu walipofika
nyumbani kwa Diamond, Sinza-Mori, Dar waliambiwa mrembo huyo alilala
hapo na kuondoka asubuhi.