Imani za kimila wilayani
Misungwi mkoani Mwanza zinadaiwa kusababisha baadhi ya wajawazito kunyweshwa
maji machafu yakiwemo yaliyofuliwa shati la mume husika anayetuhumiwa kufanya
ngono wakati mke akiwa mjamzito, kwa kile kinachodaiwa ni kuondoa mkosi ili
mjamzito husika ajifungue salama.
Katika jamii ya wenyeji wilayani
hapa, ni kwamba mjamzito anaposhiriki katika tendo la ndoa na wanaume wengi,
hupata kifafa cha mimba siku ya kujifungua na dawa yake ni kunyweshwa maji
yaliyolowekwa mchanga kutoka eneo alilowahi kuzalia mbwa.
Hayo yalielezwa katika mafunzo ya afya yanayoendelea wilayani hapa. Kuhusu
kunyweshwa maji yaliyofulia shati, Mhudumu wa Afya katika Kijiji cha Mwamanga,
Manyanda Kanyumbo alisema ikitokea mjamzito akachelewa kujifungua na
ikagundulika mumewe alikuwa na uhusiano na wake wengi, shati lake hufuliwa na
kisha mjamzito huyo hunyweshwa maji yaliyotumika.
“Watu wanaamini
akishakunywa maji machafu ya mumewe hujifungua haraka na salama na kikombe
alichonywea hufunikwa uvunguni mwa kitanda hadi atakapojifungua”, alisema.
Kwa upande wa mjamzito aliyetembea na wanaume wengi, jamii inaamini kwamba ili
aweze kujifungua salama, lazima uchukuliwe mchanga sehemu ambayo mbwa amewahi
kuzalia, ulowekwe kwenye maji na kisha mjamzito husika anywe kuondoa mkosi
kabla ya siku ya Katika mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na hospitali ya Aga Khan
kwa kushirikiana na Chuo cha Maendeleo na Ushirika cha MS TCDC kilichoko jijini
Arusha, Kanyumbo alisema, “wanaamini kabisa mwanamke ambaye amechangia wanaume
wengi, siku ya kujifungua kuna uwezekano mkubwa wa kupata kifafa cha mimba”.
Kanyumbo aliendelea kusema, “ili aweze kujifungua salama, bibi hufuata mchanga
wa sehemu aliyozalia mbwa na kuuloweka kisha humnywesha, maana tunaamini mbwa
hukutana na mbwa wengi ili aweze kutunga mimba, wale mbwa wengi huwafananisha
na wanaume wengi.”
Jacqueline Martin muuguzi wa Mwanangwa, alisema baadhi ya watu wanaamini
mjamzito akivuka mto, mtoto wake hazaliwi mapema na pia mwanamke huyo
haruhusiwi kunywa maji akiwa amesimama.
Wanadai akinywa maji akiwa amesimama siku ya kujifungua, mtoto hawezi kushuka
haraka.
Vile vile wanaamini mjamzito akikaa kwenye jiwe au kinu, mtoto huchelewa
kuzaliwa.
-- via HariLeo