Na Shakoor Jongo
MAAJABU! Jambo zito limefichuka kuwa
mastaa walio katika uhusiano wa kimapenzi, Nasibu Abdul ‘Diamond
Platnumz’ na Penniel Mwingilwa ‘Penny’ ni ndugu, AMANI limepekua na
kupata mkanda kamili.
Diamond kwa sasa ndiye mwanamuziki aliye
matawi ya juu zaidi kuliko yeyote kwenye Bongo Fleva, akisumbua vibaya
na kibao chake cha Number One wakati Penny akiingiza mkwanja kupitia
utangazaji katika kituo cha Runinga ya Dar es Salaam ‘DTV’.
ISHU YABUMBURUKA!
Sosi wa karibu, ndani ya familia ya
Diamond alinyetisha kwamba, Diamond na Penny ni ndugu wa damu lakini
jambo hilo limefahamika hivi karibuni na hivyo wanahaha namna ya kuzima
aibu hiyo.
Kwa sharti la kutochorwa jina gazetini,
sosi huyo alisema: “Ndugu kwenye familia wanagongana. Wanajaribu
kufichaficha hili jambo, lakini inashindikana. Unajua kinacholeta shida
zaidi ni kwamba Diamond na Penny watakavyokuwa baada ya uamuzi
kupitishwa.”
Alisema, pamoja na ukweli huo
kugundulika bila shaka kuwa ni ndugu, bado kuna ugumu wa wapenzi hao
waliozama kwenye dimbwi la mahaba kisha kuvunja amri ya sita, kuachana
na kubaki wakiheshimiana kama kaka na dada.
“Tatizo ni je, Diamond atakubali
kumchukulia Penny kama ndugu yake? Kama atakubali na Penny naye atakuwa
tayari? Wote kwa pamoja wanaonekana kama wanapingana na jambo hilo,”
alisema.
UNDUGU WENYEWE UKOJE?
Akieleza aina ya unasaba wa Diamond na
Penny, sosi wetu huyo alisema, bibi mzaa mama wa Diamond na bibi mzaa
mama wa Penny, wamezaliwa na mama mmoja.
Hapa anafafanua: “Kwa sababu hiyo sasa,
unaweza kuona kuwa, wale ni sawa tu na mtu na kaka yake. Tena wako ndani
ya ukoo kabisa, sema hao mabibi, kila mmoja alikuwa na baba yake,
walichangia mama tu.
“Familia imejiridhisha kabisa, halafu
isitoshe imeonekana kuwa, undugu wa kuchangia mama ndiyo wa uhakika
zaidi kuliko wa baba ambao mtu anaweza kubambikwa hata mtoto asiye wake.
Kifupi Penny na Diamond ni ndugu. Sema ndiyo hivyo historia za wazazi
wao zinashangaza mpaka basi.”
Kwa mujibu wa sosi wetu, majina ya bibi
hao wanaounganisha undugu ni Khadija Said Abas (bibi yake Penny) na Tatu
Omar (bibi yake Diamond), wote kwa sasa wametangulia mbele ya haki.
MAMA DIAMOND ACHEKELEA
Wakati jambo hilo likileta msuguano wa
kimyakimya ndani ya familia huku wengi wakitaka undugu huo uheshimiwe na
uhusiano uvunjwe kabisa, imeelezwa kuwa mama Diamond, Sanura Kassim
‘Sandra’ anafurahia undugu huo
“Kinachoshangaza sasa, mama Diamond
amefurahi sana na amezidisha mapenzi yake kwa Penny, ndiyo maana hataki
kusikia mwanaye anakuwa na mwanamke mwingine zaidi ya Penny.
“Mwenyewe anasema, kwanza undugu siyo wa
karibu sana hivyo haina madhara lakini pia anajua Diamond atampenda,
kumheshimu na hatamnyanyasa kwa sababu ni sehemu ya damu ya familia
yao,” sosi aliendelea kutiririka.
HAPA AMANI, KULE DIAMOND
Amani lilifanya juhudi za kumsaka
Diamond katika simu zake zote za mkononi bila mafanikio, likahamia
kwenye mitandao ya kijamii, likamnasa ambapo awali mahojiano yalikuwa na
kigugumizi lakini baadaye mambo yalikuwa hivi;
AMANI: Mzee vipi, mbona hupatikani kwenye simu zako zote? Kuna jambo nataka kukuuliza bwana mkubwa.
DIAMOND: Niko Nigeria. Vipi, kuna nini tena?
AMANI: Kuna stori fulani... eti ni kweli
bibi yake Penny mzaa mama na bibi yako wewe ni ndugu wa damu kwa maana
wamezaliwa na mama mmoja?
DIAMOND: Yeah but wamechangia mama, kila mmoja na baba yake.
AMANI: Kwa hiyo Penny ni dada yako kiasili si ndiyo?
DIAMOND: Yap!
AMANI: Duh! Majanga... kwa hiyo unatembea na dada yako wa damu?
DIAMOND: Nilikuwa najua basi kaka?!
AMANI: Kwa hiyo sasa baada ya kugundua hivyo, unaachana naye au?
DIAMOND: Kama nilivyokuambia, niko Nigeria... halafu niko gym sasa hivi, nitakutafuta nikitoka.
AMANI: Sawa, naomba ujibu hili swali la
mwisho. Tumesikia kuwa, mama yako anampenda sana Penny, ni kwa sababu
amegundua kuwa una undugu naye?
DIAMOND: Ha! Ha! Ha! Nikitoka gym nitakupigia simu tuzungumze vizuri.
Diamond hakufanya hivyo. Hata alivyotafutwa baadaye kwenye mtandao huo, pia hakuonekana kuwa hewani.
PENNY MIKONONI MWA AMANI
Penny alipopatikana juzi Jumanne, kwa
njia ya simu alielezwa ilivyo ambapo alisema: “Ni kweli Diamond ni ndugu
yangu wa damu. Tumegundua tukiwa tayari tumeshakuwa wapenzi.
“Hakuna jinsi tena, sanasana naona kama
mapenzi yetu ndiyo yamezidi kuimarika. Nampenda sana Diamond wangu na
sababu hiyo haitoshi kututenganisha maana kama ni makosa tayari
yameshatokea.”
MAMA DIAMOND
Kwa upande wake mama Diamond, baada ya
kusimuliwa kila kilichofika mezani mwa Amani na kutakiwa kueleza msimamo
wake alijibu kwa kifupi: “Ndiyo ni kweli unayosema, lakini kwa sasa
nipo huku Kariakoo (Dar), sipo kwenye nafasi nzuri ya kuzungumza. Njoo
nyumbani jioni, tuzungumze vizuri.”
Diamond na Penny wamekuwa kwenye penzi
lenye kasheshe nyingi kufuatia mwanamuziki huyo kuhusishwa na wanawake
wengine akiwemo aliyekuwa mpenzi wake wa zamani, Wema Isaac Sepetu.
Chanzo:Global Publishers
