HUKUMU ya kesi ya matumizi mabaya ya
ofisi katika utoaji wa kibali cha ujenzi wa jengo la ghorofa 18 karibu
na Ikulu Dar es Salaam, inayowakabili vigogo wawili wa Wakala wa Ujenzi
itatolewa Januari 15 mwakani.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Sundi Fimbo alisema hayo jana baada ya washitakiwa kumaliza kujitetea.
Washitakiwa katika kesi hiyo ambao
wamejitetea bila kuita mashahidi ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Majengo
Tanzania (TBA), Makumba Kimweri na Msanifu Mkuu wake Richard Maliyaga.
Ikulu inavyoonekana ukiwa juu ya jengo.
Awali akijitetea Maliyaga alidai kuwa,
Mkurugenzi wa Miliki wa Wakala, Charles Makungu ndiye aliyekuwa na
uamuzi wa mwisho wa kutoa kibali cha ujenzi na kupeleka barua katika
halmashauri husika na kwa waleta maombi.
Akiongozwa na Wakili Majura Magafu,
Maliyaga alidai alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kutoa Vibali na
walipopata ombi la ujenzi huo walipitia michoro na baada ya kuona ipo
sawa alisaini kibali na kupeleka kwa Makungu.
Alidai kuwa awali aliandika barua
akipendekeza ofisi ya Makungu iombe kibali kutoka Halmashauri ya Ilala
lakini hakupata majibu hadi alipopewa maelekezo kutoka katika kamati
inayoshughulikia miradi ubia kuwa watoe kibali hicho. Alidai alikataa
kutoa kibali hicho lakini baada ya wanakamati kujadili walikubali
kufuata maelekezo hayo na kutoa kibali hicho.
"Sisi hatukuhusika katika kutoa uamuzi
wa mradi huu, mimi nimeonewa kwasababu sijanufaika na sikutumia madaraka
yangu vibaya na nashangaa kwanini Makungu, watu kutoka katika kamati
yetu au ile ya miradi ya ubia hawajaletwa mahakamani," alidai Maliyaga.
Katika utetezi wake hivi karibuni
Kimweri alidai kuwa amefunguliwa kesi hiyo kwa kuwa alikuwa na ugomvi na
Waziri wa Ujenzi, John Magufuli baada ya kumchafua kwenye vyombo vya
habari.
Alidai ugomvi huo ulitokana na mchakato
wa uuzwaji wa nyumba za Serikali ambapo yeye alikataa kusaini mkataba wa
kumuuzia nyumba mwanafunzi kwa sababu hakustahili ndipo Magufuli
alipodhani kuwa alitoa taarifa hizo kwenye vyombo vya habari.
Kimweri na Maliyaga wanakabiliwa na
mashitaka matano ya matumizi mabaya ya ofisi katika utoaji kibali cha
ujenzi wa jengo la ghorofa 15 kiwanja namba 45 mtaa wa Chimara.
Aidha wanadaiwa kutoa kibali kingine cha kuongeza ujenzi kutoka ghorofa 15 hadi 18.
-habarileo