WACHUNGAJI wa makanisa mbalimbali nchini wamemkalia kooni Mchungaji
wa Kanisa la Maombezi, Antony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, kwa
kumtaka atoe rambirambi aliyoahidi mbele ya umati wa watu siku ya kuaga
mwili wa marehemu Askofu Moses Kulola Temeke, jijini Dar es Salaam hivi
karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mtu wa kamati iliyoratibu mazishi ya
kiongozi huyo wa kanisa, viongozi wote wa dini walioahidi kutoa
rambirambi hizo wametoa isipokuwa Lusekelo aliyeahidi kwa mbwembwe kutoa
shilingi milioni 15.
Katibu Mkuu wa Makanisa ya Kipentekoste
Tanzania, Mchungaji David Mwasota alisema anamheshimu Lusekelo kwani ni
mtumishi wa Mungu, lakini ni bora angetimiza ahadi yake kama
walivyofanya wenzake.
“Mzee wa Upako ni mtu mwenye jina kubwa kwenye jamii na kwa Mungu,
hivyo anapaswa kuangalia kwa undani kile anachoahidi kwa muda unaotakiwa
na amuache mke wa marehemu apumzike kwa kuwa ametokwa na mpendwa wake
na bado hana nguvu,” alisema na kuongeza;
“Haijawahi kutokea popote, mke wa marehemu akaanza kuzunguka mikoani
kukusanya rambirambi kwa walioahidi, huko ni kumsumbua, yeye atumie
hekima kuipeleka rambirambi hiyo kwa mke wa marehemu,” alisema Mwasota.
Kwa
upande wake, Mchungaji Josephat Gwajima ambaye ni mmoja kati ya
walioahidi na kutoa, alisema alitekeleza ahadi yake ndani ya muda mfupi,
kama alivyoahidi.
“Namshukuru Mungu kwani nimeweza kutimiza niliyoyatamka mbele ya watu
siku ile ya kuaga, najua nisingetoa ingenichafua pia ningeweza
kuwadhalilisha wachungaji wenzangu, nikiwa kiongozi lazima niwe mfano
bora na nionyeshe njia na uaminifu mbele ya jamii,” alisema Gwajima
aliyeahidi na kutoa kiasi cha shilingi milioni 10.
Alimtaka Mzee wa Upako kutimiza ahadi yake ili kuondoa minong’ono isiyo na tija mbele ya jamii.
Naye Mchungaji Getrude Rwakatare alisema yeye alitoa kiasi cha shilingi milioni moja aliyoahidi siku ile ya kuaga.
“Nisingependa
kuzungumzia juu ya Mzee wa Upako, ila kinachotakiwa ni kutoa kile
anachokiahidi, hivyo wote walioahidi watekeleze ahadi zao,” alisema.
Naye Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la TAG, Askofu Magnus Mhiche
amesema hafurahishwi na malumbano juu ya rambirambi na alishauriwa
kusiwepo mabishano kwa kitu kilichotamkwa wazi mbele ya jamii.
Na mke
wa marehemu, Elizabeth Kulola alisema kwa sasa amekuwa mzee asiyeweza
kutembea kutoka Mwanza kwenda Dar kufuata rambirambi kwa Mzee wa Upako
ama tu yeyote.
“Licha ya uzee lakini ni aibu kuanza kutembelea mikoa mbalimbali
kukusanya rambirambi kwani walioahidi ni wengi na kutoa ni moyo na wala
siyo deni,” alisema na kuongeza:
“Namuomba Mzee wa Upako awatume viongozi wa kanisa lake waniletee au
atume mtu yeyote anayemwamini au nimpe namba ya akaunti yangu
azitumbukize humo, sijapata taarifa yoyote toka kwake kunihitaji niende
kwake na hata ningepata isingewezekana kutokana na uzee.”
Awali Mzee wa Upako alimtaka mama huyo kufuatilia rambirambi ofisini
kwake Ubungo Kibangu jijini Dar na wala asimtume mtu yeyote hata kama ni
mtoto wake.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa kanisa mwenye wafuasi wengi, katika hali
ya kushangaza, alikataa kutimiza ahadi yake kwa maelezo kuwa baadhi ya
viongozi wa dini wamemdhalilisha, licha ya kushindwa kuainisha.
