JESHI la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, linamshikilia Philemon
Ng’ambi, mkazi wa Madale Kata ya Wazo, jijini Dar es Salaam kwa tuhuma
za kumuua mkewe, Enea Kagine kwa kumshambulia kwa mawe na matofali hadi
kumuua.
Philemon anadaiwa kufanya unyama huo kwa marehemu mkewe aliyekuwa
amebakiza siku mbili kabla ya kujivungua usiku wa kuamkia Jumamosi
iliyopita nyumbani kwake Wazo-Hill.
Akisimulia mkasa huo kwa mapaparazi wetu, jirani wa wanandoa hao aliyejitambulisha kwa jina la Fikiri Rashid alisema:
“Mimi
nyumba yangu na yao zinatazamana hivyo siku ya tukio majira ya saa tisa
usiku, nilianza kumsikia marehemu akipiga mayowe ya kuomba msaada
akisema mumewe anamuua.
“Nilitoka nje kwa lengo la kutaka kutoa msaada lakini nilihofia
maisha yangu hivyo ilinibidi niwaite vijana wa ulinzi shirikishi ambao
baada ya muda walifika eneo la tukio na kumkuta mtuhumiwa akivunja
vyombo vya ndani kama mtu aliyechanganyikiwa, wakati huo tayari alikuwa
ameshamuua mkewe.
“Baada ya kuwaona ulinzi shirikishi, alikimbilia chumbani na kwenda
kujificha uvunguni kwenye kitanda huku watoto wao watatu wakiwa
wamelala.
“Bila kuchelewa, askari wa ulinzi shirikishi walimkamata na
kuwasiliana na Askari wa Kituo cha Polisi cha Wazo ambao walifika eneo
la tukio na kumtia mbaroni mtuhumiwa pamoja na kuuchukua mwili wa
marehemu kwa ajili ya taratibu za kipolisi,” alisema Fikiri.
Kufuatia tukio hilo la kusikitisha wanahabari wetu walifika katika
Hospitali ya Mwananyamala ulipohifadhiwa mwili wa mwanamke huyo na mtoto
wake waliyemtoa akiwa amefia tumboni.
Miili hiyo ilizikwa Jumatatu iliyopita (Novemba 25) mwaka huu katika kaburi moja kwenye Makaburi ya Madale, Dar es Salaam.