MOYO huhifadhi mengi mazito hasa ya kuumiza! Staa mkubwa wa sinema za
Kibongo, Jacqueline Wolper Massawe amejikuta akimwaga machozi wakati
akianika siri tano nzito kuhusu mapenzi katika mahojiano (exclusive
interview) na Amani kwa takriban saa mbili.
Katika ‘intavyu’ hiyo iliyofanyika Jumatatu iliyopita kwenye Ofisi za
Global Publishers, Bamaga-Mwenge jijini Dar kuanzia saa 8:44 alasiri
hadi saa 10:44 jioni, Wolper alifunguka vitu vingi.
KISA/MKASA
Akizungumza kwa masikitiko, uchungu na majuto, Wolper
alisema hawezi kumsahau mwanaume huyo ambaye ni Abdallah Mtoro ‘Dallas’
kwa namna alivyomwingia kijanja na kutaka kumvunjia heshima aliyoijenga
karibia miaka kumi nyuma.
ALIANZIA WAPI NA DALLAS?
“Siku ya kwanza Dallas alinipigia simu
na kuniambia aliniona Magomeni (Dar). Naikumbuka sana siku hiyo, ilikuwa
baada ya mizunguko yangu, mwanzoni sikupokea simu yake kwa sababu
ilikuwa namba ngeni kwangu.
“Nilimsikiliza sana. Jamani yule
mwanaume anaongea kwa ushawishi wa hali ya juu mno. Nilishangaa
aliponieleza kila kitu kuhusu familia yangu na nyumbani kwetu. Kumbe
tayari alishaunda urafiki na baba yangu (mzee Massawe).
“Mwanzoni nilidhani ni tapeli. Nikamkatia simu. Akaendelea kunipigia
na nilipoona imekuwa kero kubwa nilipokea. Ili kuthibitisha anawajua
wazazi wangu, alinitajia namba zao za simu ambazo ni za kweli.
“Pamoja na hilo nilimfanyia nyodo, si unajua mtoto wa kike? Lakini aliniongelesha kwa upole hadi nikapunguza nyodo zangu.
“Aliniuliza nataka anifungulie biashara gani. Nikamwambia biashara ya
nguo. Akaniuliza nataka mtaji kiasi gani. nikamwambia dola laki moja
kwa sababu nilikuwa sitaki fremu moja, nilitaka nyumba nzima. Akaniambia
hakuna tatizo.
“Pia aliniuliza naishi wapi? Nikamwambia Sinza (Dar) alionesha dharau kwenye simu akaniambia atanihamishia Mbezi Beach.
“Aliniuliza natembelea gari gani? Nikamwambia Toyota Noah. Akaniambia
ningependa aninunulie gari gani? Nikamjibu Toyota Discovery lakini yeye
akasema ataninunulia Toyota Harrier.
“Kweli baada ya siku mbili-tatu nililetewa Toyota Harrier nyeusi
nyumbani. Niliogopa isijekuwa mtego nikaingia kwenye matatizo hivyo
nilimzungusha mtu aliyeniletea hadi Sinza-Mori nikamwambia apaki kwenye
kituo cha teksi, nikaenda na dereva nikalichukua hadharani ili lolote
likitokea nipate msaada.
“Nilikabidhiwa funguo za lile gari na documents zake, nikaondoka nalo
hadi nyumbani kwangu. Kesho yake Dallas alimtuma mtu aniletee dola za
Kimarekani 15,000 (zaidi ya Sh. milioni 24). Nilipouliza za nini
aliniambia ni kwa ajili ya shopping ya kutembelea Harrier niachane na
zile swaga za kwenye Noah (fedha inaongea). Kisha akanitumia cheni ya
dhahabu.
“Siku iliyofuata alinitumia Sh. milioni 15 nipeleke nyumbani
nikawaambie wazazi nimepata mchumba ambaye angeenda kujitambulisha
baadaye. Niliwaambia ni Dallas ambaye walikiri kumfahamu kwa sababu
alishawapigia simu na kujitambulisha kuwa ni mkwe wao.”
AMESHAKUTANA NA DALLAS?
“Hadi hapo nilikuwa sijamuona Dallas kwa sura na fedha nilikuwa natumiwa kila siku.
“Wakati hayo yakiendelea akaagiza nihamishiwe Mbezi Beach na kununuliwa lile gari lililoibua mzozo BMW X6.
“Nakumbuka siku niliyokabidhiwa lile gari nililia sana. Sikuamini macho
yangu kwa sababu Dallas aliniambia amenitumia kazawadi kumbe ni BMW X6
(lina stori ndefu inakuja)!
“Kumbuka mwanzoni nilikuwa na boyfriend ambaye tulipendana sana
lakini hatukupanga kufunga ndoa. Nilimweleza kila kitu akakubaliana na
mimi japokuwa aliumia.
“Maskini! Kuanzia hapo nikawa nimeachana na
yule boyfriend wangu lakini hakukuwa na namna kwa sababu niliamini
nimepata mchumba wa kunioa.
ATAKIWA KUBADILI DINI
“Baadaye Dallas aliniambia nimeshakuwa
mchumba wake hivyo nibadili dini. Kweli nilibadili nikawa Muislam na
jina langu likawa Ilham. Hicho kilikuwa kipindi kigumu sana maishani
mwangu kwa sababu nilionekana ni muasi katika dini yangu ambayo mama ni
mzee wa usharika na mwimba kwaya, baba ni mtu wa kanisani sana.”
NINI KILIFUATA?
“Siku moja nilikuwa Tanga nashuti filamu,
nilikuwa nikitoka hapo niende Morogoro. Dallas alinipigia simu
akaniambia yupo Nairobi (Kenya) anakuja Tanzania. Nilimwambia nipo Tanga
akaniambia atanifuata kule. “Niliendelea kupiga mzigo. Zilipita saa
nyingi, baadaye nikiwa na kruu yangu, Dallas alinipigia simu akaniambia
ameniona.
“Nilikataa, akaniambia namna nilivyo, nguo nilizovaa na watu niliokuwa nao, alipatia. Kumbe alikuja na Toyota Prado.
WOLPER MORO, DALLAS DAR
“Tulipomaliza kurekodi Tanga tulikwenda
Morogoro, yeye aliniambia anaelekea Dar. Tulikuwa tunawasiliana.
Nilipomaliza kurekodi Moro nilirejea Dar. Hapo ndipo vituko vikawa juu
ya vituko.
“Niliambiwa mara kaonekana sehemu akiwa na mwanamke au wanawake. Mimi
sikujali kwa sababu nilipomuuliza aliniambia hatuwezi kuonana kwa
sababu kipindi hicho alikuwa katika swaumu hivyo akionana na mimi
nitamharibia. (ulikuwa mwezi mtukufu).
BADO HAWAJAKUTANA?
“(Mguno) Hapo bado hatujakutana lakini yupo mjini na amejaa tele kwenye kumbi za starehe.
“Baada ya kumaliza swaumu, siku moja aliniambia anakuja nyumbani Mbezi
Beach. Niliwaalika marafiki zangu tukapika vyakula, tukafanya usafi na
kufukiza udi chumbani. Nilitandika mashuka meupe kitandani na kujipara
kisha nikavaa ushungi kuanzia mchana nikakaa kama malkia nikimsubiri
mchumba.
“Huwezi amini, hadi giza linaingia Dallas hakutia mguu. Nilipataje
aibu kwa rafiki zangu waliotaka kumuona huyo mchumba? Ninyi acheni tu!
“Nilipomuuliza aliniambia alipata dharura kuna biashara alikuwa anafanya
HATIMAYE WAKUTANA LAKINI…
“Nilikasirika sana, nikasema huyu ni
mchumba gani asiyetaka kuja kwangu? Nikampa muda wa siku tatu aje
nyumbani na alete nguo zake zote. Kweli, siku ya tatu, asubuhi
nilimsikia mtu akiita ‘Ilham Wolper Dallas’. Nilishajua sauti yake
kupitia simu hivyo nilimkaribisha na nguo zake nikaingiza ndani. Lakini
cha kushangaza alikuja na pikipiki!
“Alishinda nyumbani siku hiyo maana kuna ndugu zake walikuja.
Hatukufanya chochote. Dallas aliishia kunibusu shavuni kisha jioni
akaondoka.
“Mjini kukawa hakukaliki. Natumiwa picha akiwa na
wanawake tofautitofauti. Mmoja wa wanawake hao niliambiwa eti ana
‘ngoma’! Jamani hii dunia ina kichaa!
“Muda ukasonga, vitimbi vikawa vingi. Dallas simuoni. Muda wa kukaa
kwenye ile nyumba uliisha hivyo nikahama na nikamwambia akachukue nguo
zake.
UCHUMBA WAVUNJIKA, SASA ANAPUMZIKA HAPA
“Baadaye uchumba
ukavunjika tena mimi ndiyo nilimwambia simtaki tena. Nilikaa muda hadi
baadaye nilipopata mwanaume wangu wa sasa. Anani-control vizuri kwa
sababu kanipita umri na ana busara. Tunapendana sana. Najuta kumfahamu
Dallas. Siwezi kusahau tukio hilo katika maisha yangu. Dallas alicheza
na hisia za moyo wangu. (akaangua kilio) Niliteseka sana. Ni Mungu tu
anajua…
VIPI KURUDIA UKRISTO?
“Nimekaa muda siendi kanisani. Nilikuwa
najifungia ndani nalia kama mama yangu alivyokuwa anafanya. Siku moja
nilimwambia mwanaume wangu akaniambia kuliko kulia kila siku bora nirudi
kanisani. Ndipo nikarudia ukristo. Kwa sasa nasali Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kijitonyama, Dar,” alisema.
MBALI NA DALLAS
Kwa mara ya kwanza Wolper alikubali kuorodhesha listi ya wanaume aliowahi kuwa nao kimapenzi kwa kuwachambua mmoja mmoja.
ALI KIBA
Bila kupepesa macho, Wolper alikiri kuwa msanii wa Bongo
Fleva, Ali Saleh Kiba ndiye aliyemfundisha mapenzi: “Ni kitambo kidogo.
Wote hatukuwa mastaa lakini yeye alifanikiwa kuchomoka. Kabla ya Ali
(Kiba) nilikuwa na mwanaume lakini hatukuduu kwa maana ya utu uzima,
ilikuwa yale ya kitoto. Lakini Ali ndiye hasa aliyeniingiza kwenye
ulimwengu wa mapenzi.
KWA NINI WALIACHANA?
“Ali akawa staa. Alipokwenda nje nikasikia
wanawake wanamshobokea. Sasa mimi sikutaka karaha nikakaa pembeni lakini
jamaa ni mtu poa sana na tukikutana tunasalimiana freshi kabisa.”
DIAMOND VIPI?
“Ni kweli niliwahi kuwa na Diamond (msanii wa Bongo
Fleva, Nasibu Abdul). Tulikuwa na uhusiano lakini pia alikuwa mshirika
wa kibiashara (hataki kuitaja). Yeye alikuwa hawezi kulala bila kuniona,
lakini tulikaa kama mwezi mmoja, kwa sasa amebaki kuwa rafiki yangu na
siyo mpenzi tena kama zamani,” alisema Wolper.
VIPI KUHUSU JUX?
“Jux (msanii wa Bongo Fleva, Juma Khalid)
nilikuwa naye kabla ya Dallas na yule mwanaume wangu niliyeachana naye
wakati wa Dallas. Katika maisha yangu nilimpenda sana Jux. Siyo marioo
ni mwanaume mtafutaji aliyejiamini. Kwa sasa sipo naye. Dallas pia
alichangia mimi kuachana na Jux,” alimalizia Wolper ambaye kwa sasa ana
mwanaume asiyependa kumwanika.