Polisi
mkoani Pwani inachunguza kundi la watu linalodaiwa kuweka magogo
barabarani kuzuia msafara wa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM
(UVCCM) taifa, Sadifa Juma Khamis (MB) katika eneo la Tondoroni,
wilayani Kisarawe, mkoani humo.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, Ulrich Matei, alisema atazungumzia suala hilo baada ya kupata taarifa kamili.
Kwa
mujibu wa watu walioshuhudia tukio hilo, kundi hilo liliweka magogo
hayo jana usiku katika barabara ya kati ya eneo la Mpuyani katika njia
panda ya barabara iendayo vijijini kuingia barabara kuu ya Morogoro.
Mashuhuda
wa tukio hilo walisema katika nyakati tofauti kundi hilo lilianza
kuzuia msafara huo kwa kutaka kushinikiza dai la mgogoro wa mipaka kati
ya eneo la Jeshi la Wananchi wa Ulinzi Tanzania (JWTZ) na makazi ya watu
katika eneo la Tondoroni, wilayani humo.
Watu
hao ambao idadi yao haikuweza kufahamika walidaiwa kutishia kuchoma
moto magari ya msafara huo wa mwenyekiti wakati alipotaka kushuka na
kuzungumza nao na kuamua kujisalimisha kwa kuingia ndani ya gari na
kurudi Kisarawe.
Mwenyekiti
huyo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Donge, Tanzania Visiwani mapema
akiwahutubia wananchi wa Kisarawe aliwataka kudumisha amani kwa
kukiweka Chama Cha Mapinduzi madarakani. “Amani ikivurugika hakuna
atakayekuwa salama, hata askari nao hawatokuwa salama”.
Akiongea
na viongozi wa CCM na UVCCM katika jengo la ofisi za CCM wilaya,
aliwataka wanachama hao kuvunja makundi ya kampeni kwa kuwa hayana tija
kwa sasa, isipokuwa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Alisema kuwa Muungano wa Tanzania ni muhimu hivyo changamoto zilizomo ndani yake zitafutiwe muafaka kwa njia ya amani.
Alisema
kuna baadhi ya watu wakorofi ambao wanadai muungano uvunjwe hasa
kutoka Pemba wakidai kuwa kisiwa hicho ni chao wakati visiwa hivyo vya
Pemba na Zanzibar havina wenyewe na watu walioko huko wametokana na
biashara ya utumwa na wengi wao walitoka upande wa Tanzania Bara wa
makabila mbalimbali.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo alimsimika mwandishi wa siku nyingi,
Abubakar Mlawa kuwa kamanda wa UVCCM wilayani humo na wengine 15
wakiwamo madiwani kuwa makamanda wa UVCCM wa kata zao.
CHANZO: NIPASHE