MKAZI wa Buhare, Manispaa ya Musoma, Patrick Wambura (33) ambaye ni
mwalimu wa kujitegemea Shule ya Sekondari Makoye, anashikiliwa na Jeshi
la Polisi mkoani Mara kwa tuhuma za kuiba mtoto wa kike wa miaka
minne.
Mwalimu huyo alifanya wizi huo Novemba 15 mwaka huu maeneo ya Nyasho
stendi kwenye mgahawa wa Anastazia Hitra (28) anayedaiwa kuwa mama
mzazi wa mtoto huyo.
Akizungumza na waandishi wa habari Anastazia alidai kuibiwa mtoto
aliyemtaja kwa jina la Aisha Nelson (4) akiwa naye kwenye mgahawa huo
na kueleza kwamba mtuhumiwa alikwenda hapo kupata supu na chapati.
Anastazia alisema wakati akifuatilia malipo yake kwa mteja huyo,
ndipo alipogundua mtoto hayupo na kuanza kumtafuta ambapo alifanikiwa
kumpata maeneo ya zahanati umbali wa mita 500 kutoka mgahawani hapo
akiwa na mtuhumiwa aliyekuwa anajiandaa kupanda pikipiki.
“Nilipomuona akiwa na mwanangu nilipiga yowe kuomba msaada kwa
wananchi ambao walinisaidia kumkamata huyo mwizi ila mtoto wangu
alikuwa salama,” alisema.
Jeshi la Polisi linaendelea kumshikilia mtuhumiwa na kwamba
atafikishwa mahakamani muda wowote baada ya upelelezi kukamilika.