MSHIRIKI pekee wa kiume aliyeingia katika fainali ya Shindano la muziki la Epiq Bongo Star Search, Emmanuel Msuya amefanikiwa kunyakuwa kitita cha Tsh 50milioni, baada ya kumbwaga Elizabeth Mwakijambile katika hatua ya fainali, awali washiriki wote watano walianza kwa kuimba nyimbo zao wenyewe ambapo Emmanuel aliimba wimbo wa (leo ni leo), wakati Elizabeth Mwakijambile akiimba wimbo wa moyo unadunda.
Katika hatua ya pili washiriki wote walipata nafasi ya kuimba nyimbo za wasanii wengine kutoka sehemu mbalimbali duniani ambapo Amina Chibaba akaimba wimbo wa (Mwansiti),Elizabeth Mwakijambile akaimba wimbo wa (Awilo Longoma Kalolina), huku Emanuel Msuya akiimba wimbo wa (mapenzi kitugani uliopigwa na bendi ya Diamond Muzika), Maina Thadei akaimba wimbo wa (Miriam Makeba unaotwa Patapata), na Melisa John akaimba wimbo wa (Maria Cary unaitwa Heroe).
Hatua ya tatu ikawatupa nje Amina Chibaba na Maina Thadei, huku Elizabeth Mwakijambile,Emmanuel Msuya na Melisa John, wakiingia katika hatua ya tatu bora, ambapo waliendelea kuchuana vikali huku Emmanuel ambaye alionekana kuwa na mazingira mazuri zaidi ya kunyakuwa kitita cha Tsh 50milioni, akikabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Melisa John na Elizabeth Mwakijambile.
Nyota ya Emmanuel ilianza kuonekana mapema, hasa baada ya majaji wa fainali hiyo wakiongozwa na Chief Jaji Madam Ritha pamoja na Master J ,Banana Zoro na Fid Q kuonyesha kuwa Emmanuel anakila dalili za ushindi katika shindano hilo.
Raundi ya mwisho ambayo ilimtupa nje ya mashindano hayo mshiriki Melisa Jonh ambaye alitokea Ukonga jijini Dar es Salaam na kumwachia ulingo wa kutafuta mshindi wa Tsh50milioni, Emmanuel Msuya na Elizabeth Mwakijambile kati ya washiriki watatu walioingia katika hatua ya tatu bora na kuingia katika fainali, ambapo Emmanuel Msuya kutoka Mwanza, akaibuka mshindi wa BSS mwaka 2013 baada ya kuimba wimbo wake wa mwisho wa Ben Paul unaoitwa maneno maneno na kumbwaga Elizabeth Mwakijambile kutoka Dodoma.