NYOTA wa Tamthiliya ya Jumba la Dhahabu,
Miriam Nyafulwa Jolwa ‘Jini Kabula’ aliwahi kunywa sumu ambayo
haikujulikana mara moja huku chanzo kikiwa ni ugomvi wa kimapenzi na
mzazi mwenzake, Tuesday Kihangala ‘Chuz’.
Akizungumza na mwandishi wetu mwanzoni
mwa wiki hii, Chuz alisema tukio hilo lilijiri mwaka 2011 nyumbani
kwake, Makongo jijini Dar na kwamba siku hiyo hataisahau kutokana na
jinsi alivyochanganyikiwa na hali ilivyokuwa.
Aidha, Chuz alisema walikuwa na ugomvi
mdogo tu wa kimapenzi jambo ambalo alitarajia kuwa lingeisha kwa amani.
Lakini tofauti na matarajio yake, kila dakika iliyokuwa ikiondoka Kabula
alizidi kupandisha mori kama si maruhani.
Alisema muda mfupi baadaye, Jini Kabula
alivunja vioo vya gari lake kwa kutumia mawe kitendo kilichompa sababu
Chuz kumpeleka polisi (hakutaja jina la kituo).
Hata hivyo, Chuz aliendelea kushusha
‘vesi’ kuwa baada ya siku mbili, Jini Kabula alitolewa kwa dhamana huku
yeye akidhani kuwa yameisha lakini Kabula aliendeleza ‘libeneke’ ambapo
alifika nyumbani kwake na kujifungia ndani kisha akanywa dawa ambazo
zilidaiwa kuwa ni sumu kali.
“Nilipokuta mlango umefungwa nilianza
kubisha hodi bila mafanikio. Niliamua kwenda polisi, wakaja na kuvunja
mlango na kumkuta akiwa amelala chali huku akiwa anatokwa na povu jingi
kinywani,” alisema Chuz.
Baadaye walimpa huduma ya kwanza kabla
ya kumkimbiza hospitali (jina tunalo) kwa matibabu zaidi. Hata hivyo,
baada ya kutibiwa, Chuz aliomba yaishe kwa amani.
“Kaka sitaisahau siku hiyo, ilikuwa mbaya sana kwangu. Jini Kabula alikuwa kabadilika kabisa, alidhamiria kujiua kweli.
“Nashukuru hamkupata habari hiyo lakini ilinichanganya sana,” alisema Chuz.
Mwandishi alimtafuta Jini Kabula kwa
njia ya simu ili kuthibitisha juu ya habari hizo ambapo baada ya
kusomewa madai hayo alianza kwa kucheka na kujibu:
“Duh! Wewe ni kiboko, umezipata wapi hizo habari? Lakini sipendi kuzungumzia mambo ya zamani, muulize vizuri aliyekwambia.”
