KAMATI ya Utendaji Simba ‘iliyoridhia
kujiuzulu’ jana usiku kwa mara nyingine ilikutana ghafla kwa ajili ya
kuweka msimamo wa pamoja, kabla ya kutoa ‘tamko zito’ leo ambalo ndilo
litakaloamua mustakabali wa klabu hiyo. Juzi usiku, pia kamati hiyo
ilikutana kwa ajili ya kuweka mambo sawa, kwani wanaamini wao ndiyo
wanaoweza kuiangamiza au kuibeba Simba kwa sasa. Kufanyika kwa kikao
hicho, kumethibitishwa pia na Kaimu Mwenyekiti wa Simba, Joseph
Itang'ale ‘Mzee Kinesi’ aliyekiri, kila kitu kitajulikana leo, pale
watakapoweka mambo hadharani.
Kamati hiyo ‘iliamua kumuweka mtu kati’
Ismail Aden Rage waliyemsimamisha uenyekiti bila mwenyewe kuwepo, huku
tuhuma zake moja baada ya nyingine zikichambuliwa kwa kina. Novemba 19,
kamati hiyo ikiongozwa na Itang’are ilimsimamisha Mwenyekiti wa klabu
hiyo, Ismail Aden Rage kwa kile kilichodaiwa kwenda kinyume na katiba ya
klabu hiyo ikiwemo kuahirisha mkutano wa kujadili katiba ya klabu. Hali
hiyo ya kusimamishwa ilitokea huku mwenyekiti huyo akiwa hayupo nchini
jambo ambalo lilionekana kama kinyume cha katiba, huku baadhi ya
wanachama wakipinga kitendo hicho. Mara baada ya kurejea Rage, aliuambia
umma kuwa kikao kilichomsimamisha hakina mamlaka yoyote hivyo
ataendelea kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo mpaka uchaguzi utakapofanyika.
Mzee Kinese alisema, katika kikao cha jana usiku watajadili mambo
mbalimbali yakiwemo mwenendo mzima wa timu yao ikiwemo kukaa kambini
pamoja na kumjadili kocha wao mpya Zdravko Logarusic raia wa Croatia
ambaye Rage hamtaki. “Kesho (leo), majibu yatapatikana juu ya hatma ya
Simba pamoja na mgogoro uliopo baina ya mwenyekiti wetu na Kamati ya
Utendaji ambayo itajadili mambo mengi ikiwemo kuiweka timu
kambini,”alisema. Alisema, katiba ya Simba inasema, mwenyekiti, makamu
mwenyekiti au mjumbe yoyote wa Kamati ya Utendaji kama watendaji hao
hawapo na uwezo wa kuongoza kikao, ambacho kina uwezo wa kumsimamisha
mjumbe yoyote kama amekwenda kinyume na matakwa ya klabu. Kutokana na
kifungu hicho anasema, Rage hajaonewa na hana uwezo wa kutoitambua
Kamati ya Utendaji ya Simba kutokana na ‘maamuzi’ waliyoyafanya.
Alisema, anaamini mambo yote yatakwenda sawa na mgogoro utamalizika ili
kuweza kuijenga timu ambayo itaweza kufanya vizuri katika mzunguko wa
pili wa Ligi Kuu Bara. Rage ambaye ametakiwa na TFF kuitisha mkutao mkuu
wa Simba kabla ya siku 14 na kukataa, hivi sasa yupo Uingereza ambako
amedai anakwenda ‘kula kuku’