Wakati Kenya, Rwanda na Uganda zimeunda umoja unaoitwa `Umoja wa Walio Tayari’ , Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) nazo zimeanzisha ushirikiano baina yao.
Katika siku za karibuni kumekuwa na mtikisiko
ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) baada ya Tanzania na Burundi
kutengwa na wenzao wa Kenya, Rwanda na Uganda katika baadhi ya masuala
muhimu ya ushirikiano hasa wa kiuchumi.
Tanzania, Burundi na DRC nazo zimekutana ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi ya Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Samuel Sitta ambaye aliliambia Bunge lililopita kuwa Tanzania inafikiria
kushirikiana na nchi hizo.
Mkutano wa ujirani mwema
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya
mkutano wa Ujirani Mwema uliofanyika mjini Bujumbura, Burundi jana,
Sitta alisema Tanzania, Burundi na Kongo zimekubaliana kuendeleza
miundombinu ya barabara, reli, anga na usafiri wa maji katika Ziwa
Tanganyika.
Alisema mkutano huo ulilenga kuboresha miundombinu
ya usafiri katika Ziwa Tanganyika ambalo linaziunganisha Burundi
Tanzania, DRC na Zambia.
“Pia tumepanga kuendeleza reli ya kati kutoka eneo
la Uvinza, Tanzania hadi Msongati, Burundi na pia kuunganisha Barabara
ya Manyoni - Tabora - Kigoma kupitia Bujumbura hadi Kivu ya Kusini,
DRC,” alisema Sitta.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Sitta pamoja na Waziri
wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Burundi, Leontine Nzeyimana na
Waziri wa Uchukuzi wa DRC, Jack Lukeba.
“Pia tulitembelea Bandari ya Kalindo iliyoko
katika Ziwa Tanganyika upande wa Burundi kwani tunataka kuboresha
bandari za ziwa hilo,” alisema Sitta.
Waziri huyo alisema Tanzania na Burundi
zitaunganishwa na Barabara ya Manyoni – Tabora - Kigoma na Barabara ya
Manyovu - Mgina, Mabanda - Bujumbura itakayounganishwa mpaka Kivu ya
Kusini, DRC.
Kuhusu usafiri wa anga, Sitta alisema nchi hizo
zinaangalia uwezekano wa kuanzisha safari za ndege za Dar es Salaam
mpaka Bujumbura.
Muungano wa Walio Tayari ------Mwananchi