Search in This Blog

WATANZANIA WAENDELEA KUKAMATWA KWA MADAWA YA KULEVYA, WENGINE WAWILI WANASWA AFRIKA KUSINI

Watanzania wawili wanahojiwa na Polisi wa Afrika Kusini baada ya kukamatwa jana na kilo 55 za dawa za kulevya.
Watu hao wawili wanatazamiwa kufikishwa mahakamani kesho kujibu tuhuma za kukamatwa na dawa hizo zenye thamani ya Rand75 milioni (Sh11.7 bilioni).   Maofisa wa Kikosi Maalumu cha Kupambana na Makosa ya Jinai na Rushwa cha Afrika Kusini (The Hawks), kiliwakamata watu hao katika Kitongoji cha Kempton Park, Ekurhuleni, Jimbo la Gauteng.
Msemaji wa Hawks, Paul Ramaloko alisema jana kuwa maofisa hao walivamia nyumba waliyokuwa wanaishi Watanzania hao na kukuta mzigo huo. 
Hata hivyo, alikataa kutaja majina ya watu hao kwa kuhofia kuharibu uchunguzi akisema bado walikuwa wanawasaka watuhumiwa zaidi wakiwamo raia wa Afrika Kusini.
Alisema kikosi chao kimepata mafanikio makubwa kwa kukamata dawa nyingi kiasi hicho... “Tunakaribia kuwakamata vinara wa biashara hiyo, maana tumeelezwa kuna kundi kubwa la watu wazito,” alisema Ramaloko. Hii inakuwa mara ya pili katika kipindi cha miezi minne kwa Watanzania kutuhumiwa kubeba dawa hizo.
Julai mwaka huu, wasanii wawili Agness Gerald `Masogange’ na Melissa Edward walikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Oliver Tambo, Johannesburg wakiwa na kilo 180 za kemikali aina ya ephedrine zenye thamani ya Sh7 bilioni.
Baada ya kukaa miezi miwili jela, Masogange alipatikana na hatia ya kuingiza kemikali hiyo, ambayo hutumika kutengeneza dawa za kulevya na kutozwa faini ya Rand 15,000 (Sh2.3 milioni).
Melissa aliachiwa huru baada ya kuonekana hana hatia.
Wasafirishaji sasa watumia samaki
Katika hatua nyingine, wasafirishaji wa dawa za kulevya inasemekana wamebuni mbinu mpya ya kutumia samaki kusafirisha bidhaa hiyo haramu.
Akizungumza jana wakati wa uteketezaji wa dawa za kulevya, Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa za Kulevya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Godfrey Nzowa alisema wanatumia samaki kwa kuwa wana harufu kali.  
--Mwananchi
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger