Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji hicho, Maganga Kasope, tukio hilo lilitokea Oktoba 28, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi na kusababisha zaidi ya kaya mia sita kukosa mahali pa kuishi.
Mwenyekiti huyo akiwa na majonzi, alisema katika tukio hilo akina mama watatu waliokuwa wajawazito, walijifungua kwenye mbuga za mpunga wakati wakikimbilia kijiji cha jirani cha Mwamkulu kujihifadhi. Kujifungua kwa akina mama hao kulisababishwa na uchovu walioupata wakati wakikimbia moto.
Mmoja wa wahanga wa tukio hilo, Daudi Lulehiwa ,28, alisema tukio hilo liliwalazimu wao na watoto wao wadogo ketembea umbali mrefu kuelekea kijiji cha jirani cha Mwamkulu huku wakiwa wamebeba mizigo yao.
Alisema mkewe aitwaye Kulwa Elias (24) aliyekuwa na ujauzito wa miezi minane, alijikuta akijifungua akiwa chini ya mti wakati akikimbia lakini mtoto wake alifariki muda mchache tu baada ya kuzaliwa.
Naye Mchungaji wa Kanisa la P.A.G wa Kijiji cha Mwamkulu, Petro Mahega alisema wahanga hao waliofika kijijini hapo kujihifadhi, wamekuwa wakiishi kama wanyama na familia zao.
Alisema wamekuwa wakiishi chini ya miti na hivi karibuni walinyeshewa mvua wakati wa usiku, jambo lililomlazimu kutoa jengo la kanisa lake ambalo ni dogo ili litumike kuwahifadhi.
Mhanga mwingine, Maridadi Gwachele (72) mwenye familia ya watu 20, wote wakiishi chini ya mti, alisema hivi sasa wameanza kupata magonjwa ya kuambukiza, ikiwemo kuharisha.
Alisema hali hiyo inatokana na maji wanayokunywa pamoja na mazingira machafu wanayoishi na kwamba watoto ndiyo waathirika wakubwa.
Mdae Masanja alisema mbali ya kuchomewa nyumba yake pia amepoteza chakula kilichoteketea kwa moto baada ya kushindwa kukihamisha kwenye nyumba yake wakati ikiungua.
Alisema sasa hivi wanalala nje bila hata kujali jinsia za familia walizo nazo kutokana na tukio lenyewe kuwalazimu kulala kwa kuchanganyika na wamekuwa wakijisaidia kwenye vichaka.
Mhanga mwingine Katali Ngeleja aliliambia gazeti hili lililofika kijijini hapo kuwa, watoto wenye umri kati ya miaka 7-8 walipotezana na familia zao kwa muda wa siku mbili.
Aliongeza kuwa, mwenzao aliyekuwa na mashine ya kusaga alishuhudia ikiungua moto na kuteketea bila msaada wowote.