KIJANA aliyefahamika kwa jina la Abdul Kiba amejikuta katika wakati
mgumu baada ya kukamatwa akiwa na simu inayodaiwa kuwa ni ya wizi na
‘kuswekwa’ sero kufuatia jitihada za ndugu zake kumuwekea mdhamana
kugonga mwamba, Ijumaa limetonywa.
Tukio hilo lilijiri Jumanne ya wiki hii katika viwanja vya Karume jijini Dar, wakati kijana huyo alipokuwa akicheza mpira.
Kwa
mujibu wa chanzo chetu makini kilichokuwa uwanjani hapo, muda mfupi
baada ya mchezo huo kumalizika, ndipo Abdu akawekwa chini ya ulinzi wa
polisi wa kituo cha Msimbazi, kwa tuhuma ya kuwa na simu ya wizi aina
ya Samsung Galaxy yenye thamani ya shilingi laki nane, ambayo inadaiwa
kuwa mali ya mfanyabiashara aliyetajwa kwa jina la Abdallah Muhidini.
Katika mahojiano yake na Polisi, Abdul alijitetea kuwa simu hiyo
aliuziwa na vijana wawili siku za hivi karibuni aliowataja kwa majina ya
Shaaban Rajab au Kibabu kama anavyojulikana kwa wengi (anayeshikiliwa
na polisi).
Hata hivyo licha ya utetezi huo, Abdul alifunguliwa kesi jalada Na. MS/RB/12267/2013 WIZI KUTOKA MAUNGONI.
Akizungumza na mwandishi wetu kwa njia ya simu, Kaimu Kamanda wa
Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, ACP Juma Bwire alithibitisha
kukamatwa Abdul Kiba na kwamba upelelezi bado unaendelea.