Search in This Blog

ANZA MWAKA 2014 NA FIKRA MPYA

KUNA wakati unafikiria kufanya kitu fulani muhimu kwa ajili ya yule uliyemteua kuwa mwenzi wa maisha yako? Je, huwa unafikiria kama upo katika uhusiano sahihi au unakwenda tu mradi siku zinakwenda?
Wapo watu ambao wako tu kwenye uhusiano kabla ya uchumba lakini matukio kibao yametokea.

Wameshafumaniana, wameshapigana, wameshatoleana maneno machafu, wameshadhalilishana nk. Je, ni sahihi kuendelea katika uhusiano huo? Jibu ni jepesi kabisa, si sahihi.
Ndugu zangu ni vizuri kutafakari. Utakuta mtu yupo kwenye urafiki kwa miaka mitano na mpenzi wake, hajatambulishwa wala hakuna dalili za kufanyika jambo hilo. Siyo sawa. Acha kupoteza muda wako.
Uchumba wa miaka mitano (ikiwa hakuna vikwazo muhimu) si sahihi. Ni muda ambao wenzako tayari wameshakuwa na watoto wawili! Jaribu kutafakari. Usikubali kupoteza muda wako kwa jambo ambalo halina uelekeo.
Wakati unaanza mwaka huu mpya ndugu yangu, pata muda wa kutafakari kuhusu uhusiano wako. Je, kuna matarajio? Je, mwanandoa wenzako analandana sawa na wewe au kuna dalili za kusalitiwa? Kaa utafakari na uchukue hatua.
Anza mwaka huu ukiwa na matumaini mapya, mawazo mapya na fikra mpya kuhusu maisha yako yajayo. Acha kuhesabu namba za siku, wiki, miezi na miaka kila siku ukibaki palepale.
Hapa kwenye All About Love, tutaangalia mambo muhimu ya msingi na kutazama kwa undani uhusiano ulivyo ili uweze kujua upo kwenye kundi gani na kuchukua hatua haraka.

Achana na mazoea, usikubali maumivu katika moyo. Usikubali kuingia mwaka huu ukiwa bado unaburuzwa tu. Tathmini, alikufanyia nini katika kipindi chote cha uhusiano wenu?
Tazama hata katika mwaka huu pekee, amefanya kipi cha kukufanya umuone bado yu bora katika maisha yako? Inawezekana juzi tu kwenye Sikukuu ya Krismasi alikutesa na kukunyanyasa moyo wako, angalia kwa makini.

Lazima awe na umuhimu kwako, awe ameonesha kweli anakupenda na anaweza kuwa nawe katika maisha yako ndipo ukubali kwa moyo wako kuendelea naye katika mwaka huu. Hebu twende tukaone zaidi katika vipengele nilivyowaandalia.
KWENU WANAWAKE
Dada zangu, mnapoangalia mtu muhimu wa kuwa naye katika maisha ni muhimu sana kuangalia tabia zake, fanya tathimini ya jumla, kutafuta kujua kama ni kweli ana sifa za kuwa na wewe.
Kumfanya awe wako, maana yake umempa nafasi kubwa katika moyo wako. Sasa hakuna sababu ya kumpa moyo wako mtu ambaye penzi lake lina mashaka. Hapa nimekuandalia sifa za mwenzi ambaye hafai kuwa wako.

Soma kwa makini, ikiwa katika mapito ya penzi lenu ana nusu ya sifa nitakazotaja hapa, ni bora utulie, ikiwezekana utafakari upya kuanza mwaka mpya ukiwa katika mtazamo wa tofauti.
Hatimizi ahadi...

Mwanaume ambaye ana nia ya kukutumia na kukuacha, unaweza kupima hata maneno yake, mara zote amekuwa mtu wa maneno mengi ambayo hayatekelezeki! Ahadi zake zimekuwa nyingi ambazo baadaye unagundua kwamba ni hewa.
Huyu hana mapenzi ya kweli na nia yake ni kukuchezea na kukuacha na ndiyo maana anaweza kuropoka hata mambo ambayo anajua wazi kwamba hana uwezo wa kuyatekeleza. Mchunguze zaidi mwanaume wa aina hii, kwani ni moja kati ya dalili za mwanaume ambaye hana sifa ya kuwa na wewe.
Hana mipango...
Hataki kabisa kuzungumzia juu ya mustabali wa maisha yenu ya baadaye. Hataki mijadala ya mambo ya ndoa, ukianzisha anakukatisha. Hata mijadala hiyo inapotokea kwenye runinga au redio mkiwa naye, atabadilisha channel ili asisikilize au kuona.

Huyu bado yupoyupo, anapendezwa na uzuri na mwonekano wako ambao kwake ni pambo la muda tu, na siyo la kudumu kama ambavyo wewe unawaza. Hana mpango na wewe.
Uhusiano wa siri...
Hataki uhusiano wenu ujulikane na ndugu zake/zako wa karibu. Hata inapotokea akalazimika kufanya hivyo, hutoa visingizio vingi. Anaogopa kukutambulisha kwa sababu anafahamu wazi kwamba hana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye badala yake anakutumia tu!

Huyu hafai kabisa kuwa mwenzi wako na unatakiwa kumfuta katika akili yako.
Bado kuna mengi ya msingi zaidi ya kujifunza, wiki ijayo tuendelea na vipengele vingine, USIKOSE!
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger