USHIRIKINA.
Katika hali inayotafsiriwa kuwa ni imani za
kishirikina, mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Merry Patrick au
Mama Jack, mkazi wa Magole B Ilala jijini Dar es Salaam, ametoweka
kimiujiza nyumbani kwake usiku wa manane wiki iliyopita.
Chacha Muhochi, mume wa mwanamke huyo, aliliambia gazeti hili kuwa
siku ya tukio, saa tisa usiku akiwa nje ya nyumba akilinda mifugo yake,
aLimwacha mkewe amelala ndani, ghafla alisikia sauti ya mtoto wake wa
mwisho akilia, hali iliyomfanya akimbilie ndani kutazama kilichotokea.
Baada ya kuingia ndani, alishangaa kutomuona mkewe kitandani kwani
mtoto alikuwa peke yake. Alipojaribu kuchunguza, mlangoni mwa nyumba
yake, aliona damu. Aliingia katika vyumba vyake vyote pasipo kumuona
mkewe huyo, ambaye pia alikuwa ni mwanakwaya wa SDA.
“Sikujua nini kilimkuta mke wangu, nilihangaika kila kona sikumuona,
nikaona niende kwa mjumbe na kutoa taarifa polisi, hadi ninavyozungumza
na wewe bado hajaonekana,” alisema Chacha na kuonesha hati ya Polisi
(RB) STK/RB/23241/2013.
Lakini katika hali ya kushangaza, baadhi ya majirani na waimba kwaya
wenzake, wanadai mwanamke huyo huwa anaonekana nyakati za usiku na
kwamba simu yake ikipigwa inaita bila kupokelewa, lakini baadaye hutuma
ujumbe usioeleweka.
Mmoja wa waimba kwaya ambaye pia ni jirani na mama Jack, alisema
wamekuwa wakikesha katika kufanya maombi kila siku, lakini wamekuwa
wakishangazwa na ujumbe wanaopata wanapojaribu kupiga simu ambayo huwa
haipokelewi.
“Tuache kwanza, kwa sasa ana majukumu, yuko bize, ila mchawi wenu
hataki akae hapa, anaweza kuja muda wowote, yuko bomba kinoma,” huu ni
mmoja wa ujumbe unaotajwa kuandikwa kupitia simu ya mwanamke huyo
anayedaiwa kutoweka kimiujiza.
Mwanakwaya mmoja alidai siku moja wakiwa katika maombezi, ujumbe
mwingine kutoka simu ya mwenzao huyo uliingia katika simu ya wanamaombi
hao na uliosomeka hivi; “Wachawi wakubwa mkiongozwa na huyo aliyejuu,
ng’ombe wakubwa nyie, pigeni magoti chini.”
Mjumbe wa shina namba saba Bi. Fatuma Juma alithibitisha kutokea kwa
tukio hilo la aina yake ambalo limewatia hofu kubwa wakazi wa eneo hilo.