Search in This Blog

FANYA MAMBO HAYA KUZUIA UGOMVI ILI MAHUSIANO YENU YAENDELEE KUDUMU MILELE, YASOME HAPA

LEO usiku wa saa sita, tutakuwa tumekaa pamoja na familia zetu na wapendwa wetu, tukiisubiri kwa hamu dakika ya kwanza ya mwaka mpya, 2014. Kama inavyotokea mara zote, tutashangilia kwa furaha sana tukio hili, maana jambo lenyewe hutokea mara moja tu kila mwaka.
Ni siku ambayo kila mtu anayebahatika kuifikia, huifurahia sana, maana Mwenyezi Mungu anakuwa amekuchagua kuwa miongoni mwa binadamu waliopendelewa, hasa ukitilia maanani kwamba wenzetu wengi, wanaofikia mamilioni, wameshindwa kuufikia mwaka huu!
Kwa kutambua kwamba tunaanza mwaka mpya 2014, nimeona ni jambo la busara kuja na mada hii kwa sababu wote tunafahamu kuwa katika uhusiano wetu wa kimapenzi na hata ndoa, mara nyingi matatizo yanayojitokeza, huonyesha dalili tokea mapema.
Wewe unamfahamu vizuri mwenza wako, mambo gani huyapenda, yapi huyachukia, chakula anachokula (kama mnaishi pamoja), aina ya mazungumzo anayopenda na kuchukia na hata aina ya mavazi yanayomsisimua. Kama hivyo ndivyo, ni rahisi kujua kitu kinachoenda kutokea.
Kwa mfano, kama mumeo amekuja nyumbani akitokea kazini akiwa amechoka, sura yake haina furaha hata kidogo, anakuja moja kwa moja na hasira zake anakaa kwenye kochi akiwa amenuna. Kwa vile unatambua tabia zake anaporudi kutoka kazini, ni wazi utaona mabadiliko makubwa.
Utatambua kwamba mwenzio amekerwa na kitu, kama siyo na wewe, basi huko kazini kwake au popote pengine. Katika nyakati kama hizi, kuwa mpole, vuta subira na anza naye mazungumzo taratibu, tena ukiwa na staha. Siyo umemuona mwenzio katika hali kama hiyo, wewe unakurupuka, ‘Nini tena? Umeshaharibu huko eeeh, au umefumaniwa?’
Kauli kama hizi zitazidisha tatizo, kwa sababu hata kama amepata matatizo kazini, njiani au popote pale, kauli hizi zitamfanya azidi kukasirika na wengine wanaweza hata kuibua jambo jipya.
Tunasema tunaweza kuzuia ugomvi baina yetu kabla haujaanza. Tunasema hivi tukimaanisha nini? Ni kwamba mume anaweza kuwa amekosea, tuseme jambo dogo tu, kama kugeuka nyuma kuangalia makalio ya mwanamke mwingine, wakati anajua ameongozana na mkewe.
Wako wanawake ambao lazima waseme jambo kwa kitendo hicho cha mumewe, tena wakati mwingine kwa hasira na sauti kubwa. Lakini wapo ambao wanaweza kuchagua kukaa kimya. Ingawa lile ni kosa kwa mume, lakini kukaripiwa kwa ukali na wakati mwingine hata mbele za watu, kunaweza kumfanya akakosa uvumilivu, akajikuta naye anakuja juu na matokeo yake kusababisha ugomvi.
Ni lazima kila mmoja awe wa kwanza kukubali makosa, hata kama siyo kweli.
Hapa nazungumzia matatizo tunayosababisha sisi wenyewe, achana na yale ya kibaolojia. Kama mwenza wako amekuja akiwa na hasira kubwa, hakuna sababu ya upande wa pili nao kulipuka. Kaa kimya, mwenza wako akishamaliza kutoa yake kwa hasira, waweza kuwa wakati wako wa kujieleza, lakini kwa sauti ya chini.

Vipo baadhi ya vitu ambavyo tukivifanya, vinaweza kutusaidia kuzuia ugomvi wa ndoa au uhusiano wetu kabla haujatokea. Vitu hivi ni pamoja na uvumilivu, utayari wa kusamehe, kukubali kukosolewa na busara katika majadiliano.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger