INAPOFIKIA nyakati ambazo watu wanafanya vitendo hatari utafikiri
hakuna serikali, athari yake huwa ni kubwa zaidi. Matokeo mabaya ni
wananchi kujichukulia sheria mkononi na kusababisha hata wasio na hatia
kuuawa kinyama.
Kabla ya kwenda mbali labda yapo maswali ya kujiuliza; Kwa nini mtu
atoe uhai wa mwenzake kwa mtindo wa rejareja? Mbona wauaji hawakamatwi?
Nini kinasababisha unyama huo haukomeshwi? Jeshi la polisi jukumu lake
ni nini?
Ni muda mwafaka kwa Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi Tanzania
(IGP), Said Mwema, kusikia kilio cha Watanzania ambao wanapoteza ndugu
zao, wengine wanajeruhiwa, huku mamia wakiishi roho mkononi kwa hofu.
Mtaa
wa Ukonga Mazizini ndiyo Chinjachinja Street, kikundi hatari kimeweka
kambi eneo hilo, kazi kuu ni kufanya uporaji wa kutumia mapanga na
nondo. Wanaua watu kikatili. Kinachoshangaza ni kwamba mtaa huo upo
Wilaya ya Ilala, ndani ya Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
HATARI ILIYOPO
Uchunguzi umebaini kuwa ndani ya
Oktoba peke yake, Watanzania nane wameuawa katika mtaa huo. Hiyo ni
wastani wa watu wawili kwa kila wiki.
Hali hiyo, imesababisha kilio
cha wakazi wa eneo hilo, kwani wamekuwa hawawezi kufanya mizunguko
kuanzia saa 1 usiku kwa hofu ya kukabwa, kupigwa mapanga na kuuawa.
“Giza linapoingia tu, hakuna mtu anaweza kukatiza mtaa huu, inabidi
kujifungia ndani maana ukitoka tu unageuzwa bucha, utapigwa mapanga na
nondo, ukinusurika kuuawa heri yako,” alisema Liadi Kimaro, mkazi wa
mtaa huo na kuongeza:
“Wakati mwingine ikitokea umemaliza shughuli
zako usiku, inabidi upige simu nyumbani kuitaarifu familia kisha unalala
hoteli, maana kurudi nyumbani ni kuhatarisha maisha.
“Kuna kipindi
hali inakuwa mbaya hata mchana, kuna watu walipigwa mapanga na kuuawa
wakati bado kweupe kabisa. Tuna kituo cha polisi lakini hawazuii unyama
huu.”
HAWA WAMESHAUAWA
Wafuatao, wamebaki majina tu, wao walishatangulia mbele za haki, waliowakatisha uhai ni watu hao hatari ambao waliwaua kinyama.
Emmanuel
Marwa aliuawa Oktoba 2 (saa 4 usiku), James Kitoma, Oktoba 5 (saa 2
usiku), Siwema Abdul, Oktoba 11 (saa 12 jioni), Samson Bernard, Oktoba
15 (saa 5 usiku) na Manyati Wiliam, Oktoba 20 (saa 3:30 usiku).
Wengine ni Maneno Yohana, Oktoba 23 (saa 5 usiku), Ramadhani
Athumani, Oktoba 29 (Saa 5 usiku), Jumbe Saadam, Oktoba 30 (saa 2
usiku).
Hata hivyo, zipo taarifa kwamba wengine watatu waliuawa katika mwezi huo lakini Uwazi halijaweza kuthibitisha madai hayo.
Waliouawa
Septemba mwaka huu ni Noel Karoto, Septemba13 (saa 11 alasiri), Daudi
John, Septemba 14 (saa 3 usiku), Herrieth Ishengoma, Septemba 23 (saa
1:45 usiku), Zawadi Bwera, Septemba 28 (saa 3 usiku) na Jacob Simba,
Septemba 29 (saa 2:20 usiku).
WALIONUSURIKA KIFO
Mwandishi Mwandamizi wa Uwazi,
Haruni Sanchawa ni mmoja wa waathirika wa unyama unaotendeka kwenye
eneo hilo, kwani alivamiwa Oktoba 12, mwaka huu, akiwa anatokea kazini
kurejea nyumbani kwake.
Sanchawa ambaye anaishi mtaa huo, alipigwa
nondo na bisibisi na kujeruhiwa vibaya sana, ingawa kwa kudura za
Mwenyezi Mungu aliweza kupona baada ya madaktari kufanya kazi nzuri ya
kupigania uhai wake.
Wengine ambao waliwahi kuvamiwa na kuachwa majeruhi ni Emmamuel
Goigoi, aliyecharangwa mapanga Oktoba 6 (saa 5 usiku), Paulo Julius,
Septemba 2 (saa 5 usiku), Abdallah Yusuf, Septemba 4 (saa 2 usiku),
Thomas John, Oktoba 7 (saa 6 usiku) na Aisha Mohamed, Septemba 8, (saa
12 asubuhi).
HII NI KUSEMA DAR SIYO SALAMA
Aliyekuwa mjumbe wa
Tume ya Katiba, marehemu Dk. Sengondo Mvungi, alifikwa na mauti
kutokana na kuvamiwa na waporaji ambao walimpiga mapanga na kumjeruhi
vibaya kabla ya kufikwa na mauti nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa
matibabu.
Hivi karibuni, yalitokea mauaji ya watu watatu maeneo ya Goba
Darajani na Kimara Suka, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, chanzo cha
vifo ni ujambazi wa kutumia mapanga, nondo na bisibisi.
Matukio hayo
na mengine mengi yanayoendelea kutikisa jiji, ukiyaweka kwenye kapu
moja, jawabu la jumla ni kwamba Dar es Salaam siyo salama.
AJABU KUHUSU DOLA
Eneo la Ukonga Mazizini,
limekuwa linashangaza wengi kwa sababu limezungukwa vikosi vya usalama
kiasi kwamba kwa akili ya kawaida, siyo rahisi kuamini kama matukio hayo
yanaweza kutokea.
Ukonga Mazizini ni jirani na kambi ya askari polisi wa Kikosi cha
Kutuliza Ghasia (FFU), Jeshi la Magereza na Jeshi la Wananchi, Kikosi
cha Anga (Air Wing) na cha Gongo la Mboto, vikosi hivyo vyote vinapakana
na eneo hilo hatarishi kwa maisha ya Watanzania.
“Mtu ukipewa ramani ya Ukonga Mazizini, unaweza kudhani ni eneo
salama zaidi la kuishi kwa sababu lipo jirani na kambi za vikosi vya
usalama lakini nashangaa sijui hao waporaji wanapata wapi kiburi, maana
hawaogopi,” alisema Job Lembeli, mkazi wa eneo hilo.
WANANCHI WALISHAKATA TAMAA
Kuonesha kwamba
wamekata tamaa, hivi karibuni wananchi ambao ni wakazi wa Ukonga
Mazizini, waliamua kuandamana mpaka Kituo Kidogo cha Polisi cha Mazizini
na kutishia kukichoma moto kwa madai kwamba hakiwasaidii. Wakiwa na
hasira kali, wakazi hao waliwatuhumu baadhi ya askari polisi wa kituo
hicho kuwa wanaendekeza rushwa badala ya kuwaokoa raia wanaoteseka kwa
mashambulizi ya majambazi wauaji.
“Tukifika kituoni kuomba mtuhumiwa akamatwe, tunaombwa shilingi
20,000 mpaka 30,000 ndipo wachukue maelezo yako na kwenda kumkamata
mtuhumiwa,” alisema mmoja wa wananchi akiwa kituoni hapo, huku wengine
wakidai:
“Tunateswa na mateja (watumia madawa ya kulevya), polisi
wanawajua lakini hawawakamati, kuna mchezo hapa, watu wanakufa, polisi
wanaangalia tu.”
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mazizini, Joseph Alexander Kabati,
alipoulizwa kuhusiana na uhalifu eneo hilo, alikiri kisha
akasema:“Wananchi ni wabishi, hawataki ulinzi shirikishi, wakiambiwa
wachangie fedha ili vijana wajitolee kulinda hawataki.”