KWANZA nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuweza kutufikisha leo tukiwa hai na afya njema.
Leo
nilizungumze kidogo shirika letu linalozalisha umeme. Ni kwamba
tutakuwa tukijidanganya kusema kwamba Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), ambalo limekuwa likilegalega kila kukicha kuamini kwamba kwa
mwendo unaokwenda nao ipo siku litapata nafuu na kufanya kazi zake kwa
ufanisi.
Pamoja
na serikali kutangaza kwamba itabadilisha muundo wa shirika hilo kwa
kulifumua na kuliunda upya, bado inaendeleza hadithi hiyo ambayo ni
dhahiri imewachosha wananchi na kuonekana kana kwamba hiyo ni ngonjera
kutokana na matatizo tunayojionea ya mgawo wa umeme.
Viongozi wote wakuu wamekuwa wakiimba wimbo huo bila kuchoka na hata
viongozi wa Tanesco wamekuwa wakisema kuwa tatizo la umeme lingekuwa
ndoto, kitu ambacho si kweli kabisa.
Niliwahi kutahadharisha kuhusu
ahadi hiyo kwani nilizingatia ukweli kwamba Tanesco muda wote wa maisha
yake limeshindwa kutoa huduma nzuri kwa wateja.
Ubaya ni kwamba kwa upande wa serikali imekuwa haichukui hatua
stahiki za kurekebisha hali hiyo. Nilijua wazi kuwa inawezekana Rais
Jakaya Kikwete alipewa taarifa zisizo sahihi naye akawa akiendeleza
ahadi zisizokwisha za wateule wake, akiwamo Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo, kwamba zitaundwa kampuni za kuzalisha,
kusambaza na kuuza umeme.
Kwa kweli kwa wapenda maendeleo wote watakubaliana nami kuwa
inashangaza kuona serikali, kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za
Nishati na Maji (Ewura), kuendelea kulibeba shirika hilo hata pale
linapothibitisha kwamba halibebeki tena.
Katika hali ya kushangaza, Tanesco inadai kwamba itapata hasara ya
shilingi 1.6 trilioni kati ya Oktoba mwaka huu na Desemba mwaka 2015
iwapo halitaruhusiwa kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 90. Ewura
inasemekana iko mbioni kuruhusu shirika hilo kupandisha bei ya umeme kwa
asilimia 68.
Kwa maana hiyo, wateja wanaotumia uniti 50 za umeme kwa mwezi na
kuendelea watapata maumivu makubwa, kwani watalazimika kulipa sh 467
kila uniti kutoka Shilingi 273 wanazokuwa wakilipa sasa. Hili ni
ongezeko la asilimia 71.
Ndiyo maana nasisitiza kwa kusema kuwa shirika hilo liachwe life,
kwani mbali na muundo wake kuwa mbovu na kulifanya liwe tegemezi kwa
serikali, pia limedidimizwa na vitendo vilivyokithiri vya wizi, rushwa,
ubadhirifu, ufisadi, urasimu na umangimeza.
Tanesco ilianzishwa kisheria ikiwa na majukumu matatu ambayo ni
kufua, kusambaza na kuuza umeme kutokana na mahitaji yaliyokuwapo wakati
ule.
Hivi sasa hakuna asiyejua kwamba mambo yamebadilika kutokana na mahitaji ya nishati hiyo kuongezeka maradufu hapa nchini.
Hivyo, majukumu matatu ya msingi ya Tanesco hayana budi
kutenganishwa. Ndiyo maana mimi nadhani na wenzangu wengi tumekuwa
tukishauri sheria mpya itungwe ili iruhusu ushindani kama ambavyo
imefanyika kwenye sekta nyingine, ikiwamo ya mawasiliano.
Mimi naamini kabisa kuwa ushindani na mafanikio yanayopatikana kwenye
kampuni za simu ukipelekwa Tanesco utasaidia kuwapa wananchi huduma
nzuri. Licha ya kushusha gharama, ushindani pia utaongeza idadi ya
wateja kutoka idadi ya sasa ambayo ipo chini sana.
Hata hivyo, wasiwasi unaibuka kwa watu wengi kuwa kutungwa kwa sheria
hiyo mpya bila kuruhusu ushindani haitakuwa na maana yoyote, badala
yake itaendeleza mfumo wa mashirika ya umma na idara za serikali
kuendelea kuwa wadeni wakubwa wa shirika hilo.
Inashangaza kuona kuwa mpaka sasa Tanesco imeshindwa kukusanya zaidi
ya shilingi bilioni 300 kutoka kwa wadeni hao lakini wanang’ang’ania
kuongeza bei ya umeme kwa wananchi walalahoi. Nazungumzia walalahoi kwa
sababu kwa vyovyote ndiyo watakaoumia pindi bei ikipandishwa.
Binafsi napenda kuiona sheria mpya ikiwabana wadeni wakubwa na wezi
wa umeme kuliko kutaka kupandisha bei ya umeme kwa wananchi walalahoi au
wateja wao ambao hawadaiwi.
Nichukue nafasi hii kuishauri serikali kupeleka muswada bungeni ili
Sheria ya Umeme, Namba 10 ya Mwaka 2008 ifanyiwe marekebisho kwa lengo
la kuondoa mazingira yanayoruhusu ukiritimba unaoshikiliwa na shirika
hilo.
Sheria hiyo iwape uhuru wazalishaji wadogo wa umeme wauze
nishati hiyo katika soko huria badala ya Tanesco pekee kama ilivyo sasa.
Tanesco wanashindwa kuelewa au wanaelewa kwamba umeme wao ni ghali na
una makato mengi sana maana kuna makato ya Ewura, kodi ya vat na makato
mengine mengi yanayomuumiza mtumiaji.
Zamani mtu wa kawaida akienda kununua umeme wa shilingi 5,000 ana
uhakika wa kukaa nao kwa siku kadhaa lakini leo kama ni mwazo wa mwezi
basi unaweza kuambulia ‘yuniti’ zisizozidi kumi, tujiulize, tunawapa
nafuu Watanzania au tunawaumiza? Ipo haja ya Tanesco kufumuliwa na
muundo wa usambazaji wa nishati hii kuangaliwa upya.
Tunajionea jinsi shirika linavyokwenda, mara mgawo wa umeme mara
tunaambiwa mgawo utakuwa historia, watu wanafanya siasa katika mambo ya
uchumi. Tanesco imulikwe na kutafutiwa dawa vinginevya dhana ya kuepuka
nishati ya miti itakuwa ni porojo tu.