Search in This Blog

KAMA NI WEWE VIMEKUTOKEA HIVI UTASEMA UMEROGWA?, SOMA HAPA KUJUA NI VITU GANI


 
NIKO chumbani kwangu nafanya mazoezi ya kucheza NGOLOLO, jasho linanitoka mwanawane, unajua tena umri umesogea lakini imekuwa muhimu hapa mjini kujua kucheza ngololo. Kila mtu anajua kucheza ngololo kasoro mimi why?
Ila kuna kitu huwa kinaniudhi sana, mnakumbuka wakati ule Marlaw alipokuwa anatupa raha kwa Kiduku, ikawa kila mtu anacheza Kiduku na mi nikaona lazima nijifunze, nikajifungia ndani wiki mbili nilipotoka hapo nilikuwa naweza kushuka nikawa mfupi kama mtoto mchanga.
Nikawa natembelea vidole tu, mbona walipata tabu mtaani, kwenye maharusi, bar au popote pale, nikimsikia tu Marlaw akiimba Pii Pii, nawasha moto, kwani umaarufu ulidumu basi, si wanamuziki wakaja na kitu kipya kinaitwa Kwaito.
Kila mtu akawa anacheza Kwaito kasoro mimi, maana ilikuwa aibu, unakuta ukumbi mzima, hata watoto wadogo wote wanaenda stepu moja, nikijitahidi kujiunga niwafuate inakuwa tabu, wakigeuka kushoto miye kulia, wakija kulia mi naenda mbele.

Nikaona isiwe tabu, nikajifungia chumbani kwangu na kupiga tizi kali la kucheza Kwaito. Mwanawane nilipozipatia kitu cha kwanza nikapanda basi nikaenda kijijini kwetu kule Iringa ndanindani na kuanza kufanya mambo yangu kwenye vilabu kila jioni.
Kule niligeuka supastaa, hata jina la ukoo wetu likapaa, ingawa  hii ishu ikaniletea bifu na supasta niliyemkuta kule kijijini aliyekuwa akitamba kwa staili yake ya Kwasakwasa, ile ya kucheza kama unakata miwa huku kiuno kinazunguka kama feni.
Niliposikia anataka kuniroga nikaona nirudi Dar. Huku nimekuta mambo yamebadilika, kuna hii kitu Ngololo, ndiyo nipo naifanyia kazi.

Ila sijui nemerogwa? Maana maisha yangu yote nimekuwa nyuma, nikijitahidi niwakute wenzangu mchezo unabadilika. Nakumbuka enzi hizo wakati wadada wote wakali wa mjini wanaweka kalikiti, demu wangu alikuwa kang’ang’ania kusuka mabutu.
Nikaona nisiendeleze aibu, heri nimuache nitafute demu wa kisasa mwenye kalikiti, ile nampata tu, hata sijaanza kutamba, mambo yakabadilika, wadada wajanja mjini wakawa wanasuka rasta, ikala kwangu.
Hata enzi hizoo wakati kila mjanja alikuwa anapigilia raizoni, mimi nilikuwa navaa safari buti. Nikajitahidi, nikajinyima, nikapata pesa ya kununua raizoni, nikiamini nitakuwa kwenye kundi la wajanja. Wiki moja baadaye, moka ndiyo ikawa habari ya mji.
Hivi karibuni, imenitokea kwenye ishu ya simu, wajanja wote wakawa na Blackberry, mimi nikawa nasota na Nokia tochi yangu, nikastrago nikanunua Blackberry.
Kwa mbwembwe, niliwatangazia watu PIN namba. Sasa nachekwa, naambiwa siku hizi mambo ni Samsung Galaxy, watu wanakutana Whatsapp, sijui Instagram, imekula kwangu tena…au nimerogwa?
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger