NINAWASALIMU kwa jina la Bwana, hasa wakati huu mamilioni ya Wakristo
kote duniani wakijiweka sawa kwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo
wa Nazareti, zaidi ya miaka 2000 iliyopita.
Sijajua
kwa nini nimeamua kuandika mada hii, ila nimejikuta tu nikiandika.
Lakini nina sababu ambayo nadhani inatosha kukushawishi hata wewe
tukajiuliza kwa pamoja. Nimewahi kukutana sana na swali hili na baadhi
ya watu wakilizungumzia kwa namna ya kukebehi, kukejeli, kusifu na
kuponda baadhi ya makabila linapofika suala la uhusiano wa kimapenzi au
maisha ya ndoa.
“Umeoa Mmachame?, umekwisha, hao watu wabaya sana aisee, hawaoni
taabu kukuua warithi mali,” mtu mmoja alimshangaa mwenzake baada ya
kumwambia kuwa mwanandoa mwenzake anatokea Kilimanjaro katika kabila
hilo.
“Hao Wangoni bwana, wape hela watafikisha, lakini mwanamke hafiki
aisee, wahuni sana hao,” mwanamke mmoja alimweleza shoga yake baada ya
kumtaarifu kwamba anajiandaa kufunga ndoa na mchumba wake ambaye ni
Mngoni kutoka Ruvuma.
“Unaishi na Mhaya? Duh, mtawezana kweli, maana hao jamaa wana majivuno?!” mwingine naye anamshangaa mwenzake.
Kwa jumla, katika jamii yetu, tunalo tatizo hili kwa kiwango kikubwa
sana, tukibaguana kwa misingi ya dini, kabila, elimu na vitu vingine
chungu mzima. Tumeacha kuzungumzia mapenzi kwa maana ya uhusiano,
tumeangukia katika kujadili vitu ambavyo havihusiki kabisa.
Rafiki yangu mmoja aliniambia kwamba alilazimika kuomba ushauri kwa
watu wazima na majirani, ili aweze kushusha presha ya mama yake ambaye
alikataa katakata mpango wake wa kuoa mwanamke anayetokea katika kabila
la Warangi, wanaotokea Kondoa mkoani Dodoma, kwa sababu ambazo
hazikumtosheleza hata kidogo.
Aliniambia kuwa mama yake alimweleza kuwa wanawake wa kabila hilo ni
watu wanaopenda sana kutumia ushirikina katika uhusiano au ndoa zao.
Nimesikia mazungumzo ya namna hii kwa miaka mingi, nimejaribu
kuchunguza kwa kuulizauliza watu wa makabila tofauti walio katika
uhusiano na hata kusoma baadhi ya tafiti, inaonyesha kuwa hakuna ukweli
wowote katika mapenzi yanayohusiana na tabia za kabila.
Hakuna uhusiano wowote kwa mfano, majivuno ya Mhaya na jinsi
atakavyoishi kimapenzi na mwanamke ambaye wako kabila tofauti. Ni kweli,
kwa nje, inaonekana kama hawa jamaa ni watu wa majivuni, lakini niwe
mkweli kuwa ninao marafiki wengi Wahaya, lakini hawana majivuno hata
kidogo.
Umalaya, ujivuni, ushirikina, uroho wa mali na vitu vingine, ni tabia
binafsi ya mtu. Kulisingizia kabila ni kutotenda haki kwa sababu kwa
mfano, wakati tukiambiwa kuwa wanaume wa Kingoni ni watu wa wanawake
sana, upo ushahidi wa wazi kwamba Ruvuma si miongoni mwa mikoa yenye
kiwango kikubwa cha maambukizi ya gonjwa hatari la Ukimwi!Usisaha kulike page yetu, bofya hapa
Mtu anapaswa kufanya uamuzi wa kuingia katika uhusiano wa kimapenzi
na mtu kwa kufuata hisia zake na jinsi mwenyewe anavyomchukulia mwenza
wake. Kuchagua kabila kama ndicho kigezo cha kuishi katika uhusiano ni
ubaguzi, kitu ambacho ni dhambi kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu.
Wengi wameshangazwa na kuimarika kwa uhusiano wao ambao awali
ulitiliwa mashaka na watu wengi. Wazee wetu vijijini wangependa tuoe au
kuolewa na watu wa kabila letu, lakini katika dunia inayojikusanya kwa
kiwango kikubwa na kuwa kijiji, fikra hizi zimepitwa na wakati.
Kitu cha msingi ni kuangalia na kuzifanyia kazi sifa unazozitaka
kutoka kwa mpenzi wako. Kama ana upungufu, mchukulie yeye kama yeye na
siyo kabila, dini au elimu yake. Mapenzi ni sanaa, ambayo ndani yake
haina ukabila, usomi wala imani!