SIYO habari tena, kwani dunia nzima inajua kuhusu kifo cha shujaa wa
Afrika, nembo ya mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi, komredi
aliyefungwa jela miaka 27 akitetea usawa baina ya wananchi wa Afrika
Kusini, Nelson Rolihlahla Mandela.
Risasi Jumamosi, kwa msaada wa
vyanzo mbalimbali, linamulika kwa undani chanzo hasa cha kifo cha
Mandela, aliyefikwa na mauti usiku wa kuamkia jana, Desemba 5, mwaka huu
akiwa na umri wa miaka 95.
Ripoti za ndani zaidi, zinabainisha kuwa afya ya Mandela ilianza
kuleta mushikeli tangu akiwa kijana na kwa mantiki hiyo, sehemu kubwa ya
maisha yake alisumbuliwa na maradhi.
UNDANI WA MARADHI YALIYOMUUA
Ripoti
za wataalamu mbalimbali kuhusu afya ya Mandela, kwa pamoja zinatoa
majibu kwamba chanzo cha maradhi ya mapafu ambayo ndiyo hasa
yaliyokatisha uhai wake ni matokeo ya ukatili aliokuwa anafanyiwa
gerezani, kipindi akiwa mfungwa wa kisiasa.
Habari zinasema kuwa
kufanyishwa kazi ngumu bila kujali afya yake, kutopewa matibabu ya
uhakika na mazingira hatari aliyoshurutishwa kuishi gerezani ni
kichocheo cha afya yake kuwa mgogoro tangu ujana hadi kifo
kilipomchukua.
“Alifanyishwa kazi za kupasua mawe, kipindi hicho
vumbi nyingi ziliingia mwilini, mahali alipolala palikuwa na vumbi,
makutano na wafungwa wengi, yalimfanya apate bakteria ambao
walimsababishia maambukizi ya Kifua Kikuu,” alisema Dk. Amos Zehlani
katika uchambuzi wake kuhusu uzorotaji wa Mandela.
Dk.
Zehlani ambaye huandika makala za afya, alichambua: “Ubovu wa mapafu ya
Mandela ulisababishwa na Kifua Kikuu ambacho alikipata gerezani.”
Daktari
huyo aliongeza: “Kuna mambo mengi husababisha maambukizi ya mapafu.
Mgandamizo wa hewa kama njia ya upitishaji oksijeni na utoaji wa kaboni
ni ndogo, kama kuna vimelea hatari vinavyoingia na kutoka kwenye mapafu
au uingiaji wa wadudu wa Kifua Kikuu.
“Kwa kazi ngumu alizokuwa
anafanya gerezani, lile vumbi, mtu anaumwa lakini hapati tiba muafaka,
kwanza ni mshangao kuona amefikisha umri wa miaka 95, amejitahidi sana,
kama mwili wake usingekuwa imara, angekufa kabla ya mwaka 1994.”
ZUMA ALIVYOLIHUTUBIA TAIFA
Usiku
wa kuamkia jana, Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, aliutangazia
ulimwengu kupitia Televisheni ya Taifa ya Afrika Kusini kuhusu kifo cha
Mandela akisema: “Mzee wetu amepumzika. Taifa letu limepoteza mtoto wake
bora. Watu wa taifa letu wamempoteza baba yao. Ameondoka kwa amani.
Akaendelea:
“Mawazo yetu yanarandana na mamilioni ya watu ambao walimkumbatia
Mandela kama mtu wao na kuona kila kitu chake ni chao, hiki ni kipindi
cha huzuni kubwa sana.
“Tuliona ndani yake kile ambacho tunahitaji na
ndani yake tuliona mengi yenye manufaa kwetu. Nelson Mandela alituweka
pamoja, kwa maana hiyo tutamkumbuka.”
AFIA NYUMBANI
Mandela alifariki dunia akiwa nyumbani kwake, Johannesburg, Afrika Kusini, baada ya mapafu yake kushindwa kufanya kazi.
Tofauti
na mara nyingine ambazo Mandela alizidiwa na kukimbizwa hospitalini,
awamu hiyo haikuchukua muda mrefu kwa nafsi kuacha mwili baada ya mapafu
kufeli.
Kwa muda mrefu, Mandela alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya
mfumo wa upumuaji, maradhi ambayo inaelezwa kwamba aliyapata kipindi
akitumikia kifungo cha miaka 27 jela.
Mara kadhaa, Mandela alizushiwa
kifo, kuna nyakati vyombo vya habari ulimwenguni vilijazana hospitalini
alipokuwa amelazwa na kuripoti hatua kwa hatua kuhusu maendeleo ya afya
yake, huku ikiaminiwa kwamba angekufa wakati wowote.
Siku zote
anayejua siri ya kifo cha binadamu ni Mungu pekee, maana akiwa nyumbani
akiendelea na matibabu madogomadogo, Mandela alifariki dunia na kuacha
mshtuko na mshangao, maana imeonekana kama ‘ameondoka kimyakimya’
tofauti na matarajio ya awali.
MANDELA NI SHUJAA WA DUNIA
Rais wa Marekani, Barack Obama, anamuelezea Mandela kama kioo kwake na kwamba alijifunza siasa kupitia kiongozi huyo.
“Jinsi
alivyoendesha harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi Afrika Kusini,
akakubali kufungwa jela kwa sababu ya kutetea haki na usawa wa wananchi
wa Afrika Kusini, ilionesha kwamba siyo mbinafsi na alipambana kwa ajili
ya wengi, hiyo ilinihamasisha kuipenda siasa,” Obama aliwahi
kunukuliwa.
Mandela alipewa Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka 1993 pia
akatajwa kama mtu wa mfano kuwahi kutokea, maana ilidhaniwa kwamba baada
ya kushinda kiti cha Urais wa Afrika Kusini mwaka 1994, angeweza
kulipiza kisasi kwa Makaburu (Wazungu) waliowanyanyasa watu weusi
nyakati za Utawala wa Ubaguzi wa Rangi nchini humo.
Kitendo cha
kutolipiza kisasi, huku akiiongoza nchi hiyo kwa miaka mitano tu kwa
haki na usawa kwa kila raia wa Afrika Kusini, ni mambo yaliyomfanya awe
na thamani kubwa duniani.
Hata uamuzi wake wa kutotaka kung’ang’ania madaraka, umemfanya awe na heshima kubwa leo.
ALIPOTOKA
Alizaliwa Julai 18, 1918 katika kabila la machifu, kwenye Kijiji cha Mvezo, mjini Transkei katika Jimbo la Eastern Cape.
Alipewa
jina la Rolihlahla ambalo kwa tafsiri ya Kabila la Xhosa maana yake ni
msumbufu, akitajwa kuwa mantiki ya jina hilo ilijionesha namna
alivyoisumbua Serikali ya Makaburu.
Akiwa na umri wa miaka nane, baba
yake alifariki na kuanzia hapo alipelekwa kulelewa na Chifu wa Kabila
la Thembu ambaye ndiye aliyeratibu ndoa yake ya kwanza.
Mwaka 1943,
Mandela alitunukiwa Shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Afrika
Kusini na ni nyakati hizo alijiunga na Chama cha African National
Congress (ANC) ambacho alikiongoza kupigania usawa wa watu weusi wa
Afrika Kusini dhidi ya ubaguzi wa rangi na hatimaye mwaka 1994 kuwa rais
wa kwanza mweusi, akishinda kupitia tiketi ya chama hicho.
Mwaka 1948, Mandela alichaguliwa kuwa Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa ANC (ANC Youth League).
Mwaka
1962, baada ya kuendesha harakati nyingi za mapambano dhidi ya ubaguzi
wa rangi, alikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuhamasisha mgomo wa
siku tatu, vilevile kusafiri nje ya nchi bila kuwa na kibali.
Mwaka
1963, nyaraka ya siri kuhusu Mandela inayoitwa Umkotho we Sizwe
ilikamatwa, ikidaiwa kwamba ilikuwa na vipengele 70 vya kimapinduzi
dhidi ya serikali.
MIAKA 27 JELA
Kutokana na
makosa mbalimbali ambayo baadaye yalikuja kumfanya atajwe kama gaidi,
yalisababisha afungwe jela miaka 27 kabla ya kuachiwa huru mwaka 1990.
Alitumikia miaka 18 kwenye Gereza la Robben Island kabla ya kuhamishiwa Pollsmoor nje ya Jiji la Capetown.
Mwaka
1988, alilazwa hospitalini baada ya kugundulika ana maambukizi ya Kifua
Kikuu, ni ugonjwa huo ambao unatajwa kuchochea maradhi ya mapafu ambayo
yamechukua uhai wake.
Februari 11, 1990, Mandela aliachiwa huru.
AANZA SIASA UPYA
Akiwa
na umri wa miaka 71, Mandela alianza upya harakati za siasa baada ya
kutoka jela ambazo zilimwezesha kushinda kiti cha urais mwaka 1994.
NDOA
Mandela
alikumbana na migogoro ya ndoa, kwani alimtuhumu aliyekuwa mkewe,
Winnie Mandela kwamba hakuwa mwaminifu, akamtaliki na kumuoa mjane wa
aliyekuwa Rais wa Msumbuji, Samora Machel, Graca ambaye aliishi naye
mpaka mwisho wa uhai wake.
Mke wake wa kwanza ni Evelyn Mase ambaye
walizaa watoto wanne kabla ya kuachana, kisha akapata watoto wengine
wawili na Winnie. Mandela, ameacha watoto watatu walio hai, kwani
wengine watatu (wote mama ni yao ni Evelyn), walifariki dunia kabla ya
baba yao.