WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo, amegoma kusafiri na Watanzania wenzake kwenda nchini
Algeria kwa daraja la kawaida baada ya kukosa daraja la kwanza, hivyo
kuahirisha safari yake kwa siku moja, Tanzania Daima limebaini.
Profesa Muhongo ambaye amekuwa
akionyesha dharau kwa Watanzania mara kadhaa, aligoma kusafiri katika
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere, Dar es Salaam Jumapili ya Novemba 24,
2013, saa 10.45 akiwa na wenzake tisa kwenda kwenye safari ya kikazi
nchini Algeria alikoenda baadaye.Moja ya kauli ya dharau iliyotolewa
hivi karibuni na Waziri Muhongo ni pale aliposema wafanyabiashara
Watanzania wana uwezo wa kuwekeza kwenye soda na juisi badala ya gesi na
pia aliwahi kuwashambulia viongozi wa dini kwa kuwaita waongo.
Uchunguzi wa Tanzania Daima uliofanyika
kwa siku kadhaa sasa, umethibitisha kwamba Muhongo alikuwa aondoke na
ndege ya shirika la ndege la Emirates namba EK 726 kutoka Uwanja wa
Ndege wa Mwalimu Nyerere kupitia Dubai kwenda Algeria akiwa na tiketi ya
daraja la kawaida bila kujua kabla ya kufika uwanjani hapo na kisha
kuanza kumfokea kila aliyekuwa anamsemesha.
“Tiketi yake na wenzake kumi ilikuwa ni
Economy Class (Daraja la Kawaida), lakini akakataa akitaka asafiri kwa
First Class (Daraja la Kwanza). Alibembelezwa na wenzake na wafanyakazi
wa Emirates na wale wa Uwanja wa Ndege lakini akagoma huku akifoka na
wenzake wakataka kuahirisha safari.
Ikawa tena ni sisi kuwaomba wasafiri ili Bwana Mkubwa (Muhongo) atafutiwe nafasi kwa daraja analotaka.
“Walimbembeleza wakamwambia kwa kutumia
‘millage’ ya safari zake watambadilishia akiwa ndani ya ndege na
kumuweka daraja la kwanza lakini alionekana ameshakuwa mkali na hakuwa
anamsikiliza yeyote.“Baadaye tulifanikiwa kuwashawishi wenzake kuendelea
na safari na yeye sijui aliondoka na ndege gani tena maana wakubwa wetu
wana mambo sana,” anasema ofisa mmoja uwanjani hapo.
Taarifa za awali kuhusu sakata hili,
ziliripotiwa siku hiyo katika mtandao wa jamiiforums.com zikieleza
kwamba kitendo cha Waziri Muhongo cha kususia safari hiyo, kiliwakera
baadhi ya wasafiri wakiwamo raia wa kigeni ambao walishangazwa na hatua
hiyo ya kiongozi wa nchi maskini inayotegemea misaada kulazimisha
kusafiri kwa daraja la kwanza, daraja ambalo viongozi wa mataifa makubwa
hawaruhusiwi kusafiri bila sababu maalumu.
Taarifa hiyo kwenye mtandao wa
JamiiForums. Com iliripotiwa hivi: “Kweli viongozi wa nchi hii wanatia
aibu, wakati mawaziri wa Uingereza wanakataa First Class, hapa kwetu
kimetokea kioja. Waziri wenu wa Nishati na Madini (Muhongo) ambaye
anazidi kutulaza na joto na giza leo amewaacha hoi Watanzania pale
alipofika mpaka Airport na akiwa anaboard akakuta anawekwa sehemu ya
abiria wa daraja la kati, baada ya kuambiwa hayuko First Class akagoma
na kutoka nje ya mlango. Wakati hayo yakiendelea kumbe ana wenzake zaidi
ya tisa wako economy na wawili Bussiness Class, ghafla nao wakaanza
kushuka.
“Hapo ndipo hekima za mmoja wa wahusika
wa Airline (Emirates) akawaomba hao waende ili yeye akabadilishe aje
kesho yake.” “Jamani kweli First Class inakushushia aibu hivi Profesa na
bado unasema maisha magumu Tanzania!? Inaonekana zile buti za bora
ulizivalia ukiwa form V na haya ndio madhara yake, mnapewa vyeo wakati
maisha yalishawapiga; mnatafuta muafaka na Yesu mkiwa madarakani,”
anaeleza mtu aliyewasilisha mada husika akijulikana kwa jina la Basiasi.
Basiasi alihoji sababu ya abiria wenzake
ambao nao walikuwa wakisafiri kikazi kutaka kushuka na kusababisha
hasara kwa serikali au wafadhili waliokata tiketi hizo. Kwa utaratibu wa
kawaida abiria anayeahirisha safari baada ya kuwa ameshaingia ndani ya
eneo la kusafiria (boarding) anaweza kupoteza kabisa tiketi au
kulipishwa fedha nyingi zinazoweza kuwa sawa na kununua tiketi mpya.
“Hebu kuweni wastaarabu, sasa wale watu
tisa walitaka kuwashusha kwa nini na kama wamekwenda, mlishindwa
kuwaambia wabaki mpaka mkaanza kuleta aibu uwanjani? Inaonekena ndege
mmeanza kupanda uzeeni; najiuliza kivipi unaletewa tiketi hata kama na
‘travel agency’ halafu unashindwa kuuliza au kukagua mpaka unaenda
uwanjani na unapewa ‘boarding pass’ bado unashindwa kukagua ipi
‘bussiness class’ na ipi ‘first class’!” anahoji Basiasi. Abiria mmoja
aliyenukuliwa na Jamiiforums alisema kwa waziri wa nchi kama Uingereza
anatakiwa kutoa maelezo ya sababu za kusafiri na daraja la kwanza (first
class) ikiwa atalazimika kufanya hivyo, vingine viongozi husafiri kwa
madaraja ya kawaida.
Wakati Waziri Muhongo akisusia ndege kwa
kukosa nafasi ya kusafiri na daraja la kwanza, baadhi ya mawaziri
wanaofanya ziara mikoani na kusafiri kwa ndege, hulazimika kuyaagiza
mashangingi yao kutoka Dar es Salaam hadi katika mikoa wanayokwenda
kufanya ziara hizo hata kama yatatumika kwa siku moja.