Klabu bingwa ya soka Tanzania, Yanga imetimua benchi lake lote la ufundi kwa kile kilichoelezwa kuwa kushindwa kuleta matunda yaliyokusudiwa katika klabu hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, Yanga imetangaza kujitoa katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yanayoanza leo huko Zanzibar.
Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu alisema jana kuwa klabu yake
imechukua hatua hiyo ili kujipanga upya kwa michuano ya kimataifa pamoja
na Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza wiki tatu zijazo.
Msemaji wa Kombe la Mapinduzi, Farouq Karim alielezea kusikitishwa na
hatua ya Yanga kujitoa katika michuano hiyo na kusema Ashanti ya Ilala
imechukua nafasi ya timu hiyo.
Njovu alisema kuwa kutokana na kupewa notisi ya kutimuliwa; Kocha
Msaidizi; Fred Felix “Minziro”, Kocha wa Makipa; Razak Siwa na Daktari
wa Timu, Nassoro Matuzya, kwa sasa Yanga haina kiongozi wa benchi la
ufundi.
Kocha Mkuu wa Yanga, Ernie Brandits alikwishatupiwa virago kwa kupewa
notisi ya mwezi mmoja, siku chache baada ya kufungwa na Simba mabao 3-1
katika mechi ya Mtani Jembe kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Siwa alisema: “Nakubaliana na uamuzi wa viongozi,
siwezi kubishana nao kwa kuwa wao ndiyo wenye uamuzi wa mwisho kuhusiana
na klabu.”
Njovu alisema kuwa kwa sasa uongozi unaendelea na mchakato wa
kuwapata warithi watakaochukua nafasi hizo haraka ili waweze kuanza
maandalizi ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika
baadaye Februari.
Yanga imepangwa kuanza ugenini na Komorozine ya Comoro kwa mechi za
kwanza zitakazoanza kuchezwa kati ya Februari 7 na 9, mwaka huu.
Hata hivyo, Njovu alisema kuwa hadi kufikia jana, makocha 45 wametuma maombi ya kutaka kuinoa Yanga.
Simba uwanjani leo
Wakati hayo yakitokea Jangwani, Simba leo inashuka kwenye Uwanja wa
Amaan, Zanzibar kupambana na AFC Leopards ya Kenya katika mchezo wake wa
kwanza wa Kombe la Mapinduzi huku mgeni rasmi akiwa Kocha wa Mkuu wa
Timu ya Taifa ya Italia, Cesare Prandelli.
Michuano ya Kombe la Mapinduzi ni sehemu ya maandalizi ya sherehe za
kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na mwaka huu itashirikisha
timu 12.
Mchezo huo wa Simba na Leopards utakaoanza saa 2:00 usiku,
utatanguliwa na ule wa wenyeji KMKM ya Zanzibar ambayo itashuka kwenye
uwanja huohuo, saa 10:00 jioni kuikabili KCC ya Uganda ikiwa ni mechi za
Kundi A.
Mechi nyingine leo jioni kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba,
itazikutanisha Mbeya City na wenyeji Cloves Stars, ambayo ni kombaini ya
Kisiwa cha Pemba.
Kaimu Kocha Mkuu wa Simba, Selemani Matola alisema jana kuwa kikosi chake kimejiandaa vizuri na matarajio ya kufanya vizuri leo.
“Timu yangu ipo tayari kwa mechi ya kwanza na kwa mazoezi tuliyofanya
naamini tutaifunga Leopards na kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele
japokuwa tunaweza kukutana na ugumu, maana kama unavyoona kuna timu
kutoka nje ya nchi hapa,” alisema Matola.
Naye beki wa Simba, Donald Mosoti ‘Musso’ alisema atahakikisha
anawakaba vilivyo washambuliaji wa AFC Leopards, Allan Wanga na Jacob
Kelly leo.
—MWANANCHI—
—MWANANCHI—