Rais Jakaya Kikwete amesema Operesheni Tokomeza Ujangili iliyositishwa kwa muda kutokana na utekelezaji wake kukumbwa na kasoro na kusababisha mawaziri wake wanne kuwajibika kisiasa, itaendelea baada ya kukamilika kwa matayarisho ya awamu yake ya pili.
Akizungumza katika salamu zake za Mwaka Mpya jana, Rais Kikwete
alisema: “Tunakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya
Operesheni Tokomeza. Ni muhimu kuendelea nayo kwani tusipofanya hivyo
majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.
“Wakati nikilihutubia Bunge Novemba 7, mwaka jana niliagiza ifanyike
sensa katika Pori la Hifadhi la Selous. Hali ni mbaya, sensa imekamilika
lakini taarifa yake inatisha. Kuna tembo 13,084 tu wakati mwaka 1976
walikuwa na tembo 109,419.”
Rais Kikwete ametoa kauli hiyo ikiwa zimepita siku 12 tangu Kamati ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilipotoa ripoti yake iliyoeleza
athari mbalimbali za operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji,
uharibifu wa mali na mauaji ya binadamu na mifugo.
Ripoti hiyo ilisababisha, Rais kutengua uwaziri wa Dk Emmanuel
Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi), Dk David Mathayo
(Mifugo na Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii),
baada ya wizara zao kutajwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa
operesheni hiyo.
Hata hivyo, Rais alisema mtindo wa mzigo wa makosa ya watumishi wa
umma kubebwa na viongozi wa kisiasa pekee, tena wasiokuwa na hatia ya
moja kwa moja, siyo sahihi. “Lazima kila mtu abebe mzigo wake
inavyostahili. Ni matumaini yangu pia kwamba katika siku za usoni
kunapotokea matatizo ya namna hii uchunguzi uwe wa kina ili wale hasa
waliohusika na kutenda makosa wawajibishwe.
“Uwajibikaji wa wana-siasa peke yao hautoshi, kwani huwaacha
waharibifu waendelee na kazi isivyostahili. Mtindo huu utawafanya
watumishi wasione umuhimu wa kutokurudia makosa. Hata hivyo, pale kwenye
ushahidi wa wazi kwamba kiongozi wa kisiasa angeweza kuchukua hatua za
kuzuia madhara lakini hakufanya hivyo lazima kiongozi huyo awajibike.”
Kuhusu umuhimu wa kuendelea na operesheni hiyo alisema:
“Tusipoendelea na operesheni hii, baada ya miaka michache ijayo
hakutakuwa na tembo hata mmoja. Zoezi la kuondoa mifugo katika mapori ya
hifadhi ya taifa litaendelea na katika awamu ya pili ya operesheni hii,
washiriki watasisitizwa kutokutenda maovu yaliyofanyika katika awamu ya
kwanza.”
Alisema tangu mwaka 2010 Serikali ilianzisha operesheni mbalimbali
kupambana na ujangili wa wanyamapori na uvunaji haramu wa rasilimali za
misitu, lakini kutokana na majangili kutumia silaha na mbinu, aliamua
kuhusisha vyombo vingine vya ulinzi na usalama na hapo ndipo ilipoanza
Operesheni Tokomeza.
“Pamoja na matatizo yake, katika Operesheni Tokomeza tumebaini
mitandao ya ujangili na wahusika kadhaa wametiwa nguvuni. Mitandao hiyo
inahusisha watu wa aina mbalimbali, wamo raia wa kawaida, watu maarufu,
watumishi wa idara mbalimbali za Serikali wakiwamo wa Idara za
Wanyamapori na Misitu,” alisema.
Alisema katika operesheni hiyo watu 1,030 walikamatwa pamoja na
silaha za kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya tembo
na nyara mbalimbali.
“Niliagiza operesheni hii isitishwe na uchunguzi ufanyike kubaini
kasoro zake sambamba na waliofanya makosa wachukuliwe hatua. Wakati
suala hilo likiendelea, Bunge likaunda kamati na matokeo yake mliyaona,
mawaziri wanne wamewajibika kisiasa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliwapa pole mawaziri hao na kuwapongeza kwa uamuzi wa
kukubali kuwajibika kwa makosa yaliyofanywa na maofisa wa chini yao,
“Wameonyesha ukomavu wa kisiasa na moyo wa uzalendo.”
Dawa za kulevya
Akizungumzia dawa za kulevya, Rais Kikwete alisema kati Januari na
Desemba 2013, kilo 1,261 za heroin, kilo tatu za cocaine na kilo 89,293
za bangi zilikamatwa na watuhumiwa 1,631 kutiwa mbaroni.
“Tupo hatua nzuri katika matayarisho ya kuanzisha Kikosi Maalumu cha
Kupambana na Dawa za Kulevya katika mwaka wa fedha 2014/15. Pia
tutaitazama upya sheria ya adhabu kwa makosa ya kufanya biashara ya dawa
za kulevya ili kuifanya iwe na meno makali zaidi,” alisema.
Akizungumzia usalama wa nchi alisema mwaka 2013 umemalizika bila kuwa
na matukio yoyote mabaya na kwamba hata uhusiano wa Tanzania na nchi
jirani unaendekea kuwa mzuri.
Pia aligusia suala la ujambazi na kueleza kuwa mwaka 2013 matukio ya
ujambazi yalipungua ikilinganishwa na mwaka 2012… “Takwimu
zinathibitisha ukweli huo, mwaka 2012 matukio ya ujambazi yaliyoripotiwa
yalikuwa 6,872 na kwa mwaka 2013 yameripotiwa matukio 6,409.”
Katiba
Kuhusu Katiba, Rais Kikwete alisema uteuzi wa wajumbe 201 wa Bunge
Maalumu la Katiba utakuwa umekamilia mwishoni mwa mwezi huu na kwamba
baada ya hapo Bunge hilo litaanza.
“Iwapo Rasimu ya pili ya Katiba itakubaliwa na wananchi, hapo
tutakuwa tumepata Katiba Mpya. Lakini, iwapo Rasimu itakataliwa ina
maana kuwa Katiba ya sasa itaendelea kutumika mpaka hapo mchakato
mwingine utakapoanzishwa na Katiba Mpya kupatikana,” alisema.
Akizungumzia Pato la Taifa, alisema limekua kwa asilimia 7.1 ukilinganisha na asilimia 6.9 mwaka jana.
Pato la Taifa
“Tunategemea kuwa mwaka 2014 Pato la Taifa litakua kwa asilimia 7.3.
Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 12.1, Desemba, 2012 hadi
asilimia 6.2, Novemba 2013. Lengo letu ni kufikia asilimia 5 mwezi Juni,
2014” alisema.
Alisema hadi Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na Dola milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012.
–MWANANCHI–
Alisema hadi Novemba, 2013, Tanzania ilikuwa imeuza nje bidhaa na huduma zenye thamani ya Dola za Marekani milioni 7,720.8 ukilinganisha na Dola milioni 7,916.6 za mwaka ulioishia Novemba 30, 2012.
–MWANANCHI–