Search in This Blog

MISHAHARA JUU


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
Serikali imeongeza bajeti ya mishahara ya watumishi wa umma katika mwaka 2013/14 kwa asilimia 26 (sawa na Sh. bilioni 982.096).

Aidha, Serikali inatarajia kuajiri watumishi wapya 61,915 na kupandisha wengine cheo 42,419 wa kada mbalimbali watapandishwa cheo.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni jana mjini Dodoma.

“Katika mwaka wa fedha 2013/14 serikali inatarajia kutumia Sh. trilioni 4.763.196 kwa ajili ya kugharamia malipo ya mishahara kwa watumishi wa serikali kuu, serikali za mitaa, wakala na taasisi za Serikali,” alisema Kombani na kuongeza kuwa: “Kiasi hiki ni sawa na ongezeko la Sh. bilioni 982. 096 ambazo ni sawa na asilimia 26 ikilinganishwa na kiasi cha Sh. trilioni 3.781.100 zilizopangwa kutumika katika mwaka wa fedha 2012/13.”

Alisema fedha hizo ambazo ni Sh. trilioni 4.763.196 kitatatumika kugharamia ajira mpya, upandishwaji wa vyeo na nyongeza za kawaida za mishahara kuanzia Julai mwaka huu.

Kuhusu malimbikizo ya mishahara, Kombani alisema hadi kufikia Machi mwaka huu jumla ya madai ya watumishi wa umma 11,820 kati ya watumishi wa 52,039 wamelipwa malimbikizo ya mishahara ya Sh. 12,603,190,843 kimetumika.

Alisema malipo ya malimbikizo ya watumishi 27,245 yenye thamani ya shilingi 16,089,986,605 yalikuwa yameshahakikiwa na yanasubiri kufanyiwa  malipo kutegemea na upatikanaji wa fedha.
“Madai ya malimbikizo ya mishahara ya watumishi 12,974 yenye thamani ya shilingi 12,588,847,207 yalikuwa kwenye hatua ya uhakiki kabla kuingizwa katika mfumo wa malipo,” alisema.

Katika mwaka wa fedha 2012/13 kima cha chini cha mshahara kiliongezeka kutoka shilingi 150,000 (2011/12) hadi kufikia Sh. 170,000 kwa mwezi. Ongezeko hilo ni asilimia 13.3.
Kamati ya Bunge imeishauri Bodi ya Mishahara na Maslahi katika utumishi wa Umma kwa kuzingatia hali ya uchumi wa nchi katika kuboresha mishahara ya watumishi wa umma.

“Kwamba kila uchumi unapoboreshwa ni vizuri pia mishahara ya watumishi ikaongeza, hasa kwa kuzingatia tija na mabadiliko ya kiuchumi na kijamii,” alisema.

Aidha, maoni hayo yaliyosomwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na utawala, Pindi Chana, aliitaka bodi kuwa makini na malimbikizo ya mishahara hewa, madeni  ya watumishi wakiwemo walimu.

Msemaji wa kambi ya Upinzani kuhusu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Profesa Kulikoyela Kahigi, alisema kwa muda mrefu walimu wemekuwa ni kada ya utumishi ambayo haitendewi haki na serikali.

“Nasema hivi kwasababu kwa miaka mingi walimu wamekuwa wakilalamika kuhusu mishahara duni lakini baadhi yao wamekuwa hawalipwi stahili zao kwa mfano malimbikizo ya mishahara, fedha za uhamisho,” alisema.

Alisema mara zote walimu kupitia chama chao wanapolalamika kupata maslahi yao serikali imekuwa ikiwajibu jeuri kuwa madeni hayalipiki na pia wanapotengaza mgomo halali kwa njia ya kuifanya serikali iwasikilize, serikali imekuwa ikikimbilia mahakamani kuzuia mgomo
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger