Search in This Blog

WANAFUNZI WAZAMA NA KUFA

WATU saba wamefariki dunia jijini Dar es Salaam, wakiwemo wanafunzi wawili wa Shule ya Msingi Kinyerezi, ambao walizama kwenye dimbwi la maji yaliyotuama wakati wakiogelea huku wakivua samaki.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi alisema kuwa wanafunzi hao wakiwa na mwenzao walifika katike eneo hilo la Mto Kinyerezi, uliopo jirani na shule hiyo kwa lengo la kuogelea na kuvua samaki kwa kutumia ndoano.

Aliwataja watoto waliokufa kuwa ni Lukuman Kulwa (10), mwanafunzi wa darasa la tatu na Omari Jaribu (9), mwanafunzi wa darasa la pili, wote wakazi wa Kinyerezi.

Alisema maiti zao zimehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili. Alisema watoto hao wawili walikufa baada ya kukwama kwenye tope, ambapo mwenzao ambaye hajafahamika jina lake, alikimbia na kutoa taarifa kwa wananchi, ambao walifika eneo hilo na kuopoa miili ya watoto hao.

Wakati huo huo, mtoto aliyetambulika kwa jina moja la Obedi (5), amekufa papo hapo baada ya kuteketea kwa moto wakati akiwa amelala chumbani kwao.

Minangi alisema kuwa moto huo ulizuka juzi saa 12 asubuhi Ukonga Banana Msikitini kwenye chumba cha mpangaji aliyetambulika kwa jina moja la Veronica (25) ambae pia anatambulika kama mama Obedi.

Alisema moto huo ulisababisha kifo cha mtoto huyo na kumjeruhi Veronica ambaye aliungua vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake pamoja na kumjeruhi mtoto mwingine aliyetambulika kwa jina moja la Sara(10) ambae aliungua mkono wake wa kulia na paji la uso na alitibiwa katika hospitali ya Amana na kuruhusiwa.

Alisema chanzo cha moto huo kinasadikiwa kwamba ni kibatari kilichowashwa na Veronica ambacho kililipuka na kusababisha moto huo kuenea kwenye chumba hicho na kuzimwa na wananchi kabla haujaenea katika vyumba vingine.

Maiti imehifadhiwa hospitali ya Amana na Veronica amelazwa katika hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Aidha mtoto mwingine wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 10 amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari katika eneo la St. Mary's wakati akivuka barabara ya Tabata.

Gari hilo lenye namba za usajili T 965 BZW aina ya Noah lilikuwa likiendeshwa na Shebe Mohamed (32). Pia Said Waziri (70), mkazi wa Ukonga amekufa papo hapo baada ya kugongwa na gari lenye namba za usajili T 190 AEH Nissan Patrol katika maeneo ya Ukonga Magereza.

Katika hatua nyingine, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Engelbert Kiondo amesema kuwa watu wawili wamefariki dunia katika mkoa wake katika matukio ya ajali.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger