WATU sita wamelazwa katika Hospitali ya DDH-Bunda, mkoani Mara,
kutokana na kujeruhiwa vibaya kwa kile kinachodaiwa ni kupigwa na
askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambao wanaendesha
operesheni ya kusaka wawindaji haramu.
Mganga Mkuu katika wodi ya wanaume hospitalini hapo, Dk. Alphonce
Kwessi, alisema kuwa majeruhi waliopokewa hospitalini hapo ni pamoja na
Diwani wa Kata ya Nyarikoba wilayani Tarime, Mustapha Mashani, wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambaye ameruhusiwa baada ya hali
yake kutengamaa.
Dk. Kwessi alisema kuwa majeruhi wengine ambao bado wamelazwa ni
pamoja na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kipaso wilayani Tarime, Robert Mrenda
(CCM), Saguda Mihayo, Makoye Kazi, Ezekiel Nyarusi na Igeye Wambura.
Alisema kuwa majeruhi hao wamefikishwa hospitalini hapo tangu Oktoba
16, mwaka huu wakiwa na hali mbaya na kwamba waliletwa na askari hao
pamoja askari wa Tanapa, wakidai kuwa wamekamatwa kwa tuhuma ya uwindaji
haramu.
Hata hivyo diwani huyo wa CHADEMA juzi alifikishwa katika Mahakama ya
Wilaya ya Bunda na kushitakiwa kwa uwindaji haramu, ambapo alipatiwa
dhamana baada ya kutimiza masharti.
Kutokana na suala hilo, Mratibu wa Mafunzo Kanda ya Ziwa Mashariki wa
CHADEMA, Chacha Heche, juzi alifika hospitalini hapo, alisema chama
chao hakiridhiki kabisa na nguvu kubwa iliyotumika katika kuwakamata
watu hao.
Heche alisema kuwa wapo watu waliokamatwa bila kuwa na vielelezo wakati wakiwa majumbani mwao, akiwamo diwani huyo.
“Haturidhishwi na nguvu kubwa iliyotumika na mamlaka inayofanya kazi
ya kusaka wawindaji haramu kiasi cha kukiuka na kuvunja miiko na
taratibu za haki za binadamu,” alisema.
Alisema kuwa wao kimsingi hawapingi zoezi hilo la kukamata wawindaji
haramu lakini inabidi liangaliwe upya, kwani nguvu inayotumika katika
kukamata watuhumiwa ni kubwa mno, ikiwa ni pamoja na watuhumiwa kupewa
adhabu za kijeshi.
“Huu ni ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu, watu wamekamatwa bila
kuwa na vielelezo, tena wengine majumbani mwao, kwa mfano diwani huyu,
lakini baada ya kukamatwa walifichwa kwenye kambi mbalimbali, wamepigwa
sana, yaani ukiwaona utashangaa, wamesema eti walikuwa wanapewa adhabu
za kijeshi,” alisema.
Polisi wilayani Bunda walithibitisha kuwapo kwa majeruhi hao, hawakuwa
tayari kutoa taarifa zaidi kwa madai kuwa ni operesheni ya kitaifa.
SOURCE .TANZANIA DAIMA