NOVEMBA 27 katika Uwanja wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), wananchi mbalimbali walikusanyika kuadhimisha siku 16 za
kupinga ukatili wa kijinsia.
Makundi mbalimbali yalishiriki wakiwemo wanafunzi, wanaharakati,
polisi, taasisi mbalimbali pamoja na watu waliokumbwa na mikasa ya
unyanyasaji wa kikatili katika ndoa zao.
Miongoni mwa waliokuwepo katika umati huo ni Eva Mollel (33),
aliyekuwa akitembelea magongo hali iliyoonyesha ana matatizo katika
mwili wake.
Nilimsogelea na kuanza kuzungumza naye kilichomsibu na kumsababishia kutembea na magongo hayo.
Eva anadai ulemavu huo umesababishwa na mume wake ambaye ni mfanyabiashara jijini Dar es Salaam.
Anasema katika ndoa yao wamebahatika kupata watoto watatu wa kike, mmoja ana miaka 12, mwingine saba na mdogo sita.
Eva anasema amekuwa akishirikiana na mume wake katika miradi yao
mbalimbali, ikiwemo kumiliki hoteli ijulikanayo kama Temboni Resort.
Kwa maelezo ya Eva, Agosti 10 mwaka huu alipata ulemavu huo wa kudumu
baada ya kusukumwa na mume wake kutoka ghorofani hadi chini ambapo
alizimia na kujikuta amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
(MNH).
Kisa cha tukio hilo ni pale alipomuuliza mume wake jana yake alikuwa wapi, mbona hakurudi nyumbani.
“Nilimuuliza mume wangu jana yake alikuwa wapi mbona hakurudi. Kabla
ya kujibiwa, nilipigwa ngumi ya jicho, nilivunjwa taya, kisha
nilisukumwa toka ghorofani hadi chini na kuvunjika nyonga. Nilipoteza
fahamu,” anasimulia.
Kwa mujibu wa Eva tukio hilo lilitokea katika hoteli yao ya Temboni Resort majira ya saa tano usiku.
“Madaktari walisema ‘kikombe’ kilichanika vibaya ikabidi wanipasue
waniwekee chuma. Ninakaa na chuma sasa hivi, wameniambia hakiwezi
kutolewa. Pia natembelea magongo,” anasema.
Katika ndoa yake amekabiliwa na visa vingi ila waliyamaliza kienyeji
isipokuwa tukio hilo la kuvunjika nyonga na kuunguzwa na pasi aliripoti
polisi. Lakini hawajachukua hatua stahili hadi sasa.
Tukio jingine anasimulia ni la mwaka 2007 ambapo anadai mama mkwe
wake, yaani mama wa mume wake aliyekuwa anakaa naye kipindi hicho,
alimng’ata kidole cha kati katika mkono wake wa kulia kwa tuhuma za
kuzaa na mume wake, yaani baba mkwe wake.
Anasema baada ya kufanyiwa ukatili huo, mume wake hakuchukua hatua
yoyote, alikaa kimya tu. Jambo hilo nalo likaisha kienyeji.
Eva anadai tukio jingine alilotendewa na mume wake ni pale alipomnyoa
nywele kwa kutumia kisu mwaka 2009, kisa alimwambia amwandalie supu,
na alipochelewa akamfanyia ukatili huo.
Si hilo tu, bali mwaka juzi, kutokana na malumbano yaliyotokea baina
yao, anadai kuwa mumewe alimuunguza na pasi katika mkono wa kushoto na
kwenye matiti. Anasema lengo lake alitaka kumuunguza usoni, lakini
akajikingika.
Eva anasema hadi sasa amebaki na makovu mwilini mwake, na kwa matukio
yote hayo hakuna mwanafamilia upande wa mume wake aliyesimama na
kukemea vitendo hivyo anavyofanyiwa.
“Hili la kuniunguza mwilini, siku hiyo tulikuwa na malumbano,
akatoka, aliporudi alinikuta nanyosha nguo, ndipo aliponinyang’anya
pasi na kuniunguza,” anasimulia Eva.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za
Binadamu, Helen Kijo, anasema suala la Eva wamejaribu kuwasiliana na
polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe. Hivi sasa lipo kwenye ngazi
ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC).
Pia anasema kwa kuwa ametendewa ukatili na mumewe, anatakiwa kupata
ulinzi na fidia. Vile vile watamsaidia masuala ya ndoa yake.
“Mume wake anakataa kuongea nasi, anasema tuongee na mwanasheria wake,” anasema mkurugenzi huyo wa LHRC.
Naye Kaimu Mkurugenzi Makosa ya Jinai, Kamishna wa Polisi Isaya
Mungulu, anasema tukio hilo halitaishia hapo, atahakikisha hatua
stahiki zinachukuliwa kwa mhusika.
Kwa maelezo ya kamishna huyo, baada ya kumsikiliza Eva ameona kuwa
inaonekana polisi waliokuwa wanafuatilia suala hilo wamekiuka maadili,
hivyo itakapobainika nao watachukuliwa hatua stahiki.
“Huduma yetu haikuwa nzuri na thabiti kwa Eva Mollel, kama kutakuwa
na ukweli kuwa suala lake lilizungushwa baada ya kuripotiwa,
utajulikana baada ya kulifuatilia,” anasema Mungulu.
Ofisa wa Polisi Kitengo cha Jinsia na Watoto, Makao Makuu ya Jeshi la
Polisi, Pili Nyamanditu, anasema mtandao wa polisi wanawake
ulianzishwa mwaka 2007, lengo likiwa ni utekelezaji wa kazi za polisi
katika kuelimisha askari wa kike na kiume pamoja na jamii kuhusu masuala
ya unyanyasaji wa kijinsia na watoto.
Anasema mafanikio waliyoyapata ni kuanzisha drop centers sita Dar es
Salaam. Pia wametoa elimu ya unyanyasaji wa kijinsia kwa polisi 1,047
ili waweze kushughulika na kesi za unyanyasaji wa kijinsia na watoto.
Kwa miaka miwili, 2011 na 2012 wamepokea makosa 12,161 waliyofanyiwa
watu wenye zaidi ya miaka 18; yaliyopelekwa mahakamani ni 8,962, kesi
zilizopatikana na hatia ni 4,100 na zile zinazoendelea mahakamani ni
3,512.
Kwa miaka chini ya 18, makosa yaliyoripotiwa ni 1,605, yaliyopelekwa
mahakamani ni 1,490, kesi zilizopatikana na hatia ni 723 na zile
zinazoendelea mahakamani ni 542.
Anasema changamoto wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa madawati kwani
kati ya 417 yaliyopo ni nane tu yaliyokarabatiwa ambavyo ni vyumba
viwili tu.
“Makosa ya jinai ya kijinsia yanatokea katika ngazi ya familia, hivyo
baadhi ya wanafamilia hawashiriki vyema katika vita hii kwani
huzungumza nyumbani na kuyamaliza kienyeji bila kuangalia madhara
yanayompata mtendewa,” anasema.
Pia baadhi ya mashahidi hushindwa kutoa ushahidi kwa kuogopa kuharibu uhusiano wao katika familia.
Changamoto nyingine ni mahakama za watoto kuwa chache, hivyo kufanya kesi hizo kusikilizwa katika mahakama za kawaida.
Wakati huo huo, Mwanasheria Harold Sungusia anasema takwimu za
Shirika la Afya Duniani (WHO) za 2005 zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya
wanawake Tanzania wamefanyiwa ukatili wa kijinsia.
Asilimia 31 wamefanyiwa ukatili wa kingono, asilimia 56 wamefanyiwa ukatili wa kawaida na wa kingono pia.
Anasema takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2008 huko Zanzibar zaidi ya
asilimia 43 ya wanawake na watoto hufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Sungusia anasema sheria ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977
ibara ya 13 inazungumzia usawa mbele ya sheria, kuwa watu wote ni sawa
mbele ya sheria na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote kulindwa na
kupata haki sawa mbele ya sheria.
Anasema ibara ya 13.6 (e) inasema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomdhalilisha.
Sungusia akizungumzia haki ya faragha na ya usalama, anasema kila mtu
anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake
binafsi na familia yake na unyumba wake, na pia heshima na hifadhi yake
na mawasiliano yake binafsi