KUPOROMOKA
kwa jengo la ghorofa Mtaa wa Indira Gandhi jijini Dar es Salaam Machi
29 mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 36, kunadaiwa
kutokana na uzembe wa serikali.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyotolewa Novemba 24 mwaka huu na
taasisi isiyo ya kiserikali ya Twaweza, asilimia 87 ya watu waliohojiwa,
iliitupia lawama serikali kwamba inahusika kwa kiasi kikubwa.
Asilimia 47 ya watu waliotoa maoni yao juu ya kuanguka kwa jengo
hilo, ilisema kuwa uzembe wa wakaguzi wa majengo wa serikali pia ni
miongoni mwa chanzo kingine.
Pia ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 32 ya waliohojiwa walisema
kuporomoka kwa jengo hilo kulisababishwa na kampuni ya ujenzi iliyokuwa
ikishikilia dhamana ya ujenzi wake.
Aidha, ripoti hiyo ambayo imejikita katika mahojiano ya watu 333
katika wilaya zote tatu za Dar es Salaam, inaonyesha kuwa asilimia 18 ya
maoni yaliyotolewa kuhusu sababu za kuporomoka kwa jengo hilo ni uzembe
wa manispaa husika.
Mbali ya hayo, ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 57 hawafahamu
chochote kama kuna fidia zilizokuwa zimelipwa kwa waathirika ama familia
zao.
Ripoti hiyo ya utafiti ilikwenda mbali zaidi na kubainisha kuwa maoni
juu ya suala la mgawanyo wa wajibu ni sehemu kubwa ya jukumu, ambapo
asilimia 46 ilisema wahusika hawafanyi kazi kwa kuhakikisha kuwa
sheria za ujenzi zinafuatwa badala yake imekuwa ni kinyume.
Asilima 32 ya waliohojiwa pia waliitupia lawama kampuni ya ujenzi kwa
ajali mbaya wakati ni suala la wajibu binafsi, lakini pia asilimia 78
walikubaliana kwamba rushwa ni chanzo cha majanga kama hayo.