RAIS
Jakaya Kikwete ameviagiza vyombo vya dola kuhakikisha vinamkamata mtu
yeyote bila kujali cheo, atakayebainika kumbaka au kumuoa mwanafunzi wa
shule.
Ametoa kauli hiyo huku aliyekuwa waziri wa wizara tofauti katika
awamu mbalimbali za uongozi, Profesa Juma Kapuya, akiandamwa na tuhuma
za kumbaka na kutishia kumuua binti, mwanafunzi mwenye umri wa miaka 16.
Ingawa Rais Kikwete hakutaja jina, lakini ni dhahiri kuwa kauli hiyo
inamgusa pia Profesa Kapuya, Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM).
Akizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mikutano ya hadhara kwenye
wilaya za Itilima, Meatu na Maswa mkoani Simiyu, Rais Kikwete alisema
mtu anayefanya mapenzi na wanafunzi lazima akamatwe, ahojiwe na
kufunguliwa mashitaka ya ubakaji na si vinginevyo.
“Kuna watu wanafanya mapenzi hadi na wanafunzi wakati sote tunajua
ukimwi upo na hauna dawa na unaua. Kwa hiyo kila mmoja wetu awe makini
kujikinga nao na tuepuke kuwaambukiza wengine,” alisisitiza Rais
Kikwete.
Wakati Rais Kikwete akisisitiza wahalifu wa makosa ya kubaka na kuoa
wanafunzi wachukuliwe hatua, polisi jijini Dar es Salaam wamekuwa
wakisuasua kumchukulia hatua Profesa Kapuya licha ya binti anayedaiwa
kumbaka, kufungua jalada namba OB/RB/21124/13 katika kituo cha Polisi
Oysterbay, jijini Dar es Salaam, akidai kutishiwa kuuawa na mbunge huyo.
Kauli ya Rais Kikwete imeonyesha dhahiri kukerwa na moja ya ujumbe
mfupi wa maneno wa simu ya mkononi kutoka kwenye simu inayodaiwa
kumilikiwa na Profesa Kapuya kwenda kwa binti aliyebakwa, ambapo mbunge
huyo alijigamba kwamba serikali haiwezi kumfanya chochote.
Ujumbe huo unasomeka hivi: “Mkiuawa itakuwa vizuri…itawapunguzia
gharama za kuishi, usitake kugombana na serikali mtoto mdogo kama wewe,
sisi ndiyo wenye nchi yetu, mwenye hilo gazeti ni Mbowe, sasa mwambieni
nyumba ya kuishi si mmemuingizia hela leo? Mnatumika tu bure watu
wanaingiza hela nyingi, ila mmenitibua lazima niwaue, wiki hii
haitaisha, nitapiga kambi kote, jana si wamekuficha, tuone utalindwa
milele, maana washatengeneza hela, lazima mvae sanda tu, hilo sio ombi
ni wajibu wenu, mnajitia na nyie mafia watoto siyo, watoto wetu wanauza
unga nani anawakamata? Nani atapingana nasi.”
Habari kutoka Ikulu ya Rais Kikwete zinaeleza kuwa kiongozi huyo wa
nchi amekerwa na kauli ya mbunge huyo wa Urambo Magharibi kwamba
serikali haiwezi kumfanya jambo lolote.
Ni kutokana na kauli hiyo, mtoa taarifa wetu alisema rais aliagiza
vyombo vya dola kufuatilia kwa karibu sakata hilo na kuhakikisha sheria
inachukua mkondo wake.
Pamoja na msimamo wa Rais Kikwete na binti anayedaiwa kubakwa
kuripoti polisi, Profesa Kapuya alifanikiwa kusafiri nje ya nchi huku
polisi wakimshuhudia bila kumtia mbaroni.
Akiwa nje ya nchi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura, alikaririwa mara kadhaa akijigamba kuwa polisi inamsaka mbunge
huyo na itamtia mbaroni mahala popote alipo.
Hata hivyo, Profesa Kapuya alirejea nchini juzi huku polisi wakimshuhudia bila kuchukua hatua zozote.
Mwanafunzi huyo anadai kubakwa na Profesa Kapuya kwenye moja ya
hoteli ya kitalii iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia
tena kitendo hicho ndani ya ofisi yake katika Jengo la Biashara Complex
lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012 alipomuita kwenda kuchukua ada.