Rais Jakaya Kikwete, ameviagiza
vyombo vya dola na viongozi wa ngazi mbalimbali nchini, kuanza mara moja
kufanya msako mkali wa kuwakamata watu wanaoa wanafunzi wa kike wa
shule za msingi na baada ya kukamatwa wafikishwe katika vyombo vya
sheria kwa makosa ya ubakaji.
Rais Kikwete ametoa agizo hilo wakati akihutubia
wananchi wa wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ambapo amesema vyombo vya
dola na viongozi kwa kushilikiana na walimu, wanapaswa kufanya msako huo
kwa kila mwaka na endapo watabaini kuna mtoto ambaye ameacha shule kwa
kuolewa,basi wazazi wake wabanwe na kuwarudisha watoto mashuleni kisha
kumkamata muoaji na kufunguliwa mashita ya ubakaji kwa vile umri wa
watoto hao huko chini ya mtu mzima.
Kwa upande wao baadhi ya mawaziri ambao
wameambatana na rais Kikwete katika ziara hiyo,wameelezea kazi
mbalimbali ambazo zimefanywa na zinategemewa kufanywa na serikali huku
wizara ya maji ikiahidi kutatua tatizo la maji wilayani Itilima na
wizara ya nishati na madini ikisema serikali kwa sasa inafanya kazi
kubwa ya kupeleka umeme katika vijiji 1600 kwa nchi nzima.
Katika ziara hiyo kwa wilaya ya Bariadi na
Meatu,rais Kikwete ameweza kuzindua miradi miwili ya umeme vijijini
inayotekelezwa na wakala wa umeme vijijini REA pamoja na kuzindua daraja
la Mwanuzi ambalo limejengwa kwa fedha za ndani kiasi cha zaidi
shilingi milioni 455.