SIKU hizi uovu hauchagui
pa kutua, Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima
amejikuta katika hali mbaya baada ya kulishwa sumu na mtu mwenye nia
mbaya, Risasi Jumamosi lina kisa hicho.
Akizungumza na mapaparazi
wetu kanisani kwake, Kawe, Dar es Salaam hivi karibuni, Gwajima aliweka
wazi kwamba, tukio hilo lilimtokea mwanzoni mwa mwezi huu. Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.
MCHEZO ULIVYOANZA
Mchungaji Gwajima ambaye
anasifika kwa kuwarejesha katika hali ya ubinadamu watu waliodhaniwa
wamekufa (misukule) alisema kuwa sumu hiyo aliwekewa kwenye soda
aliyokaribishwa na askofu mmoja mkuu wa kanisa kubwa nchini Tanzania
(jina kapuni).
“Siku hiyo, huyo askofu aliniita nyumbani kwake
(hakupataja jina), nikaenda nikiongozana na askofu mwingine ambaye ni
rafiki yangu.
MAONGEZI KUHUSU MUNGU NA SODA JUU
“Tulipofika, tuliongea mambo mengi ya kiroho. Baadaye akatupa soda
lakini nilipoinywa nilihisi kuna kitu ndani yake. Roho wa Mungu pia
akasema nami kuhusu hilo, palepale nilimwambia yule askofu kwamba
amenipa soda yenye sumu ndani yake,” anafunguka Gwajima kwa mara ya
kwanza kwenye gazeti hili.
“Yeye alikuwa akikataa kwamba hajaniwekea sumu kwenye kinywaji hicho lakini cha kushangaza alionekana kutetemeka sana.”
AISHIWA NGUVU, AAGA
Gwajina alisema filamu ya sumu hiyo haikuishia hapo kwani ghafla
alianza kuhisi kuishiwa nguvu jambo ambalo lilimshtua na kuanza
kubabaika.
Gwajima: “Niliondoka haraka sana huku nikimhakikishia
yule askofu kwamba sitakufa bali nitaishi kama maandiko yanavyosema kwa
kuwa naamini katika ufufuo na uzima.
MKEWE AMTAKA AENDE HOSPITALI
Akaongeza: “Wakati huo nilikuwa nikitakiwa kuja kwenye huduma hapa
kanisani, nikaingia huku tumbo likiwa linakata sana. Cha kushangaza
nikafanya maombi kama kawaida.
“Nilipomaliza huduma nilirudi nyumbani na kumwambia mke wangu. Yeye akanisihi niende hospitali lakini nilikataa.”
AENDA KUONANA NA DAKTARI WAKE
Gwajima anaendelea: “Katikati ya usiku mnene, nilisikia kitu kimelipuka
tumboni na maumivu makali yakafuatia, nilimwomba Mungu anifikishe hadi
asubuhi. Ilipofika nilikwenda kwa daktari wangu ambaye baada ya
kunichunguza aliniambia nilipewa sumu ya kuniharibu akili na si ya kufa
kama nilivyodhani.”
Mchungaji huyo aliendelea kusema kwamba, daktari
wake huyo alimwambia kwa vile sumu hiyo aliinywa kidogo dawa yake ni
kunywa maji mengi ili kuimaliza kabisa, akamtahadharisha kuwa angeinywa
kwa kiwango kikubwa na kuchelewa tiba angechanganyikiwa akili kiasi cha
kushindwa kuwa na mawasiliano mema na binadamu wenzake.
ASKOFU ALISHALIPWA FEDHA ILI AMDHURU GWAJIMA
Gwajina alisema katika utafiti wake, aligundua kuwa askofu huyo
alilipwa shilingi milioni 300 na wabaya wake ili wamdhuru kwa sumu hiyo,
lengo ni kumfanya ashindwe kutoa huduma ya kiroho katika kanisa lake
ambalo linakua siku hadi siku.
AMPIGIA SIMU ASKOFU MBAYA WAKE
“Asubuhi ya siku iliyofuata nikiwa nimepata nafuu nilimpigia simu yule
askofu nikamwambia kwa kumtania kwamba anigawie pesa kidogo katika hizo
alizolipwa,” alisema Gwajima.
AMWACHIA MUNGU
Gwajima alisema alikuwa na uwezo wa kumpeleka mbele ya sheria askofu
huyo lakini kwa vile yeye ni mtumishi wa Mungu alitakiwa aoneshe mfano
wa kusamehe kama maandiko yanavyotaka.
Hata hivyo, alisema kama
angeamua kumwanika askofu huyo ana uhakika waumini wake wangetimka
kanisani kwake na kubaki yeye na familia yake tu.