LEO
ni siku ya kuzaliwa ya Ryan Giggs ambaye alizaliwa Novemba 29, 1973,
hiyo ikiwa na maana kuwa alianza kuliona jua miaka 40 iliyopita, Gazeti
la Championi linamtakia kheri mchezaji huyo wa Manchester United, soma
stori nzuri inayomuhusu:
Ferguson alivyomsajili kimafia
Kuanzia
mwaka 1985, Giggs alikuwa akiichezea timu ya watoto ya Manchester City,
nyuma ya pazi kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Ferguson
alikuwa akimfuatilia kupitia watu wake wa kutafuta vipaji.
Baada ya
kujiridhisha kuwa Giggs anaweza kuwa chaguo zuri kwa timu yake, Ferguson
alichofanya kwa kuwa ‘dogo’ huyo alikuwa hajafikisha umri wa kusaini
mkataba, akaamua kwenda moja kwa moja kwa mama yake mzazi na
kumshawishi juu ya kumchukua mwanaye.
Ferguson akamwambia mama huyo
kuwa licha ya kuwa atakuwa mwalimu wa Giggs lakini atakuwa kama mzazi
wake, akaahidi kuwa atamuangalia ndani na nje ya uwanja, pamoja na ahadi
nyingine nyingi, mama mtu akakubali, Man United ikamnasa Giggs kilaini.
Hivyo,
Giggs alitua klabuni hapo baada ya mama yake kumkabidhi mikononi mwa
Ferguson na kuanza maisha klabuni hapo kuanzia mwaka 1987 ambapo yupo
mpaka leo.
Achapwa makofi na Ferguson
Baada
ya kufika United, Giggs akaendelea na maisha kama kawaida katika timu
ya watoto, baadaye ndipo akapata marafiki kina David Beckham, Phill
Neville, Paul Scholes, Gary Neville na wengine wengi, lakini yeye Giggs
ndiye aliyekuwa mkubwa kuliko wote katika rika la vijana hao.
Kuna siku Giggs akiwa tayari ana miaka kadhaa klabuni hapo, akawaita
wachezaji wenzake huku akiwa na rafiki yake wa kike nyumbani kwake na
kufanya sherehe kubwa, katika sherehe hiyo, wachezaji hao walifungulia
muziki kwa sauti kubwa huku wakinywa na kula kwa raha zao.
Kuna
mama mmoja ambaye alikuwa jirani yake na Giggs, akawa anasikia kila
kitu kinachoendelea, akampigia simu Ferguson na kumuelezea juu ya
wanachofanya ‘watoto’ wake, kocha huyo akamshukuru huyo mama, akawasha
gari kuelekea nyumbani kwa Giggs.
Alipofika akagonga, kijana mmoja akafungua mlango, ile anamuona mzee
huyo, akashtuka sana, kidogo amzuie kuingia ndani, Ferguson akaingia na
moja kwa moja akafika mpaka kwa Giggs, akamwambia azime muziki, Giggs
akatekeleza hilo.
Baada ya kuzima muziki, Ferguson akamgeukia Giggs
na kumnasa makofi palepale mbele ya wenzake na rafiki yake wa kike
ambaye baadaye alikuja kuwa mke wa mchezaji huyo.
“Wewe Ryan ndiyo
mkubwa hapa, unawaongoza wenzako kufanya upuuzi, huu ndiyo mwisho wa
muziki na kila mtu asambae hapa, na kesho ole wake atakayechelewa
mazoezini,” hiyo ilikuwa ni kauli ya Ferguson aliyoitoa hapo, bila
ubishi vijana hao wote wakasambaa wakiwa vichwa chini.
Maisha ya sasa
Mpaka sasa Giggs ameshacheza mechi 952 na bado ana mkataba mpaka mwisho wa msimu huu kuendelea kuitumikia Man United.
Mapema
wiki hii aliulizwa juu ya kufikiria kustaafu, lakini Giggs akasema bado
hajafikiria juu ya kustaafu kwa kuwa hiyo inategemea na mwili wake
utakavyokuwa wakati muda wa mkataba wake utakapomalizika.
“Nina machaguo mengi, nina biashara kadhaa ninafanya, nina cheti cha ukocha, hivyo naweza kuwa na chaguo moja kati ya hivyo.
“Nafikiria
pia kucheza mpaka nitakapofikisha mechi 1,000 lakini hilo litategemea
na nitakavyokuwa nikijisikia wakati huo,” anasema kiungo huyo raia wa
Wales.
Kuhusu kuyumba kwa Man United
“Nafikiri
ni suala la benchi la ufundi na wachezaji, tutakaposhinda au kufungwa
tunakuwa ni wote, taratibu muda unavyosonga ndivyo tutavyokuwa imara,”
anasema. Akielezea kuhusu umri wake wa sasa, Giggs anasema: “Nimekuwa
nikifikiria jinsi ninavyojisikia na siyo kuhusu umri, kuna wakati
wachezaji wenzangu wananiambia ninazeeka, nawajibu kuwa umri wangu ni
miaka 35 (anacheka).”
Kuonyesha kuwa bado mchango wake unahitajika,
kocha wa sasa wa United, David Moyes tayari ameshaanza kuweka wazi nia
yake ya kumpa mkataba wa mwaka mmoja Giggs.
Kama mkataba huo utasainiwa, maana yake ni kuwa ataendelea kuichezea United mpaka atakapofikisha umri wa miaka 41.
Giggs
ambaye ana urefu wa futi 5.11, amekuwa hapati nafasi mara kwa mara
katika kikosi kinachoanza, badala yake amekuwa akianzia benchi huku
akimsaidia Kocha Mkuu David Moyes kwenye benchi la ufundi.
Wakati
anachipukia, winga huyo alikuwa na kasi ya kukimbia kiasi kwamba alikuwa
tishio kwa mabeki wengi wa timu pinzani, kwa sasa ambacho amekuwa
akifanya ni kutulia na mpira kwa kuwa hana kasi kama ambayo aliyokuwa
nayo miaka ya zamani.
Jambo jingine ambalo linawashangaza wengi ni
kuwa kile kizazi chote ambacho kilimkuta mchezaji huyo kwenye klabu
hiyo, wote wameshastaafu lakini yeye bado anacheza.
Upande wa timu ya
taifa, Giggs ameichezea timu ya taifa ya Wales mechi 64 na kufunga
mabao 12, wakati ambapo timu ya taifa ya Uingereza ameichezea mechi nne
na kufunga bao moja.
“Bado anaonekana yupo vizuri, siyo mtu ambaye
ukimtazama unadhani kuwa ataacha kucheza hivi karibuni,” anasema Moyes
na kuongeza:
“Tayari ameanza kuelekea kwenye ukocha, unapoona
mchezaji anachukua maamuzi hayo maana yake ni kuwa anajua muda wa
kucheza umebaki kidogo.”