UNALIKUMBUKA vizuri lile kundi la wale vijana wa Temeke, Daz
Nundaz? Nini TMK Family, hawa madogo walikuwa balaa. Kamanda ndiyo
ulikuwa wimbo wao maarufu zaidi na uliotikisa anga lote la Bongo Fleva.
Kulikuwa na vichwa vitano vilivyotengeneza crew hii. Ferooz, Daz Baba
au Daz Mwalimu, Sajo, Larumba na Critic. Kama ambavyo imetokea kwa
makundi mengi, Daz Nundaz sasa imebakia historia.
Mmoja wa nyota
waliokuwa gumzo kundini humo ni Daz Baba, yule dogo mwenye mwili mdogo,
akisokota nywele zake katika staili ya rasta, aliyependa kutembea kwa
mikogo.
Daz alijua kuifanya kazi yake vizuri. Licha ya kufanya kazi na kundi,
lakini jamaa aliweza pia kutengeneza nyimbo zake kadhaa binafsi ambazo
zilifanya vizuri, kitu kilichosaidia sana kumpatia shoo nyingi katika
maonesho mbalimbali.
Kuna kibao kama Umbo Namba Nane aliofanya mkongwe wa Hip Hop, Fid Q.
Ni kibao kilichokamata sana na kutamba katika chati za redio mbalimbali
nchini. Aliwahi pia ‘kusumbua’ na nyimbo zake nyingine kama Wife
aliomshirikisha marehemu Ngwair, Nipe Tano aliowapa shavu Daz Nundaz,
Elimu Dunia aliokwenda sambamba na Afande Sele.
Umaarufu ulikuwa mkubwa kwa Daz Baba na kama ilivyo kwa vijana wengi
wanaojihusisha na muziki huo, akawa kipusa. Apite wapi asijulikane.
Uzuri wa mastaa wetu, wanajijua, wanajua wanatazamwa wanapopita, lakini
hawataki kujua pia kwamba vitendo vyao vinaonekana.
Bangi katika Bongo Fleva siyo jambo la ajabu. Wengi wanavuta, lakini
taratibu habari zikaanza kuzagaa mitaani kuwa Daz Baba anatumia dawa za
kulevya. Alijitahidi kukataa, lakini macho ya watu yalimuona.
Tatizo moja la watu wa Bongo Fleva, wanaamini utumiaji wa madawa ya
kulevya ni ujanja, kwamba ukitumia ndiyo utaonekana mtoto wa mjini,
asiye mshamba. Ni kwa vile tu hawajui hatima yao ya baadaye, lakini
ukweli ni kwamba hawa ambao wao wanawaona washamba, ndiyo wajanja
halisi.
Daz Baba alianza kupoteza mwelekeo taratibu, akionekana vijiweni kwa
muda mwingi, hatimaye akafanana kabisa na wale mateja tunaowaona katika
stendi za madaladala wakipiga debe.
Miezi michache iliyopita, alionekana mjini Morogoro akiwa kama mtu
aliyechanganyikiwa kabisa. Ni jambo la kusikitisha sana kugundua kwamba
mtu ambaye jamii ilimtegemea kwa burudani, mafunzo na mfano, sasa
amegeuka kuwa kituko.
Lakini kama nilivyosema mwanzo, hii inatokana na mawazo duni ya
kutojitambua kwa wengi wa wasanii wetu, fedha na umaarufu wanaoutafuta
kwa shida kubwa, huwaletea usumbufu katika maisha yao ya kila siku.
Wasanii wetu wanaposikia Chris Brown, Snoop Dog, Jay Z, Whitney
Houston au 50 Cent wanatumia madawa ya kulevya, nao hukimbilia
kujitumbukiza bila kujua kwamba wana tofauti kubwa na mastaa hao wa
Marekani kwa kila kitu.
Wenzao wana mameneja wanaojua kazi zao, wana pesa nzuri na hata
vipimo vya utumiaji wa dawa hizo. Hawajidungi tu ovyo kama wanavyofanya
wa kwetu, ndiyo maana unawasikia wakiendelea kuwepo licha ya habari zao
kuanza kusikika miaka mingi.
Nichukue tena nafasi hii kuwashauri wasanii wetu wanaoubwia unga na
kufanya mambo mengine yasiyostahili mbele ya jamii. Wao wanapaswa kuwa
vioo vya wanaowazunguka kujitazama.
Wanayo nafasi kubwa sana ya kusaidia juhudi za serikali katika
kutatua tatizo la ajira. Wanapata fedha, wawekeze katika miradi
mbalimbali ili wenzao walio vijiweni wapate ajira, kitu ambacho
kitasaidia pia kupunguza uhalifu.