Safari ya Obama ilianza Juni 26 nchini Senegal, kisha akaenda Afrika Kusini na anakuwa Rais wa tatu wa Marekani kuzuru Tanzania akiwa madarakani.
Wengine ambao walipata kufanya hivyo ni Rais Bill Clinton na George W. Bush ambao walifika nchini kwa nyakati tofauti wakiwa madarakani.
Katika ziara hiyo, Obama anafuatana na mkewe, Michelle na mabinti zao Sasha na Malia. Sababu ya ziara Akizungumzia ujio wa kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani, Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt alitaja sababu zilizomsukuma Rais Obama kuja kuwa ni kutokana na Tanzania kuwa mfano wa nchi zenye utawala bora na ustawi wa demokrasia. Nyingine ni juhudi zinazofanywa na Serikali kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo kwa mujibu wa Balozi huyo yanaivutia Serikali ya Marekani kwani yatachangia katika kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi. Eneo lingine ni kusaidia ukuaji na uendelezaji wa viongozi vijana. Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo baadhi ya vijana wake wamekuwa wanapata mafunzo ya uongozi chini ya mpango uliozinduliwa na Rais Obama mwaka 2010.