Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa muda mrefu
katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam unaonyesha kuwa biashara
hiyo inafanyika katika maeneo ya Tandika, Manzese, Vingunguti, Temeke,
Tandale, Mtongani na Keko.
Wanawake hao wamekuwa wakitumia mwanya wa kuuza
chakula kama kinga yao, huku biashara yao kubwa ikiwa ni kuuza dawa za
kulevya aina ya heroin, bangi na aina nyingine.
Mbinu hii mpya ya usambazaji wa dawa za kulevya
kwa kutumia wanawake wanaouza vyakula imeelezwa kuwa inawasaidia
wahusika wakuu, kuendesha biashara yao kwa ufanisi zaidi.
Uchunguzi umeonyesha kuwa wafanyabiashara wa dawa
hizo wameamua kuwatumia mamalishe kutokana na kuwa waaminifu na
kuhudumia wateja wengi, hivyo ni vigumu watu kuwashtukia wakiwamo askari
polisi.
Imebainika kuwa dawa hizo huuzwa kulingana na
maeneo, wakati maeneo ya watu wasiokuwa wa uwezo hupimwa kwa kutumia
kipimo kidogo zaidi kwa bei ya chini ambayo watumiaji husika huweza
kuimudu.
Aidha dawa hizo hufungwa katika mitindo miwili
tofauti, ukiwa katika unga wa vidonge na wa kawaida ingawa bei zake
hazitofautiani sana.
Uchunguzi unaonyesha kuwa vidoge huuzwa vikiwa vizima au vipande, huku unga wa kawaida ukiuzwa kwa kipimo maalumu.
Kwa kawaida ‘unga’ huo huuzwa kwa Sh1,000 kwa
pointi huku kete moja ikiuzwa kwa Sh2,000, wakati vidonge, kizima huuzwa
kwa Sh2,000, huku kipande huuzwa kwa Sh1,000 zikitofautiana kulingana
na maeneo.
Gazeti hili lilifanikiwa kuongea na baadhi ya wanawake wanaojihusisha na uuzaji wa dawa hizo.
Dada mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Asha
(28) ambaye siyo jina lake halisi ni muuzaji mkubwa wa dawa hizo. Awali
alikuwa akifanya shughuli zake hizo za uuzaji katika maeneo ya Yombo
Kilakala, ingawaje hivi sasa amehamia Temeke.
“Unajua siku zote dhumuni la kufanya biashara ni
kupata faida, hivyo naweza kusema niliingia kwenye biashara hii kwa
sababu tu ina faida zaidi kuliko biashara nyingine,” anasema.