Jumamosi iliyopita (September 21) ndiyo ilikuwa siku ya fainali za kumtafuta mrembo wa Tanzania katika Redd’s Miss Tanzania 2013 tukio lililofanyika katika ukumbi wa Mlimani City na mrembo Happiness Watimanywa ndiye aliyetwaa taji hilo.
Historia fupi ya mrembo huyo Happiness Watimanywa:
Miss Tanzania Happiness Watimanywa mwenye miaka (19) anatokea katika familia ya Mr Louis Roussos ya Morogoro. Elimu yake aliipata katika shule mbalimbali ikiwemo Laureatte International School ya Dar-es-salaam ambayo ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kupata exposure mbalimbali za kutoka nje ya nchi kimasomo akiwa na wanafunzi wenzake.
Familia ya Miss Tanzania 2013 Happiness
Akiwa katika shule hiyo aliwahi kwenda katika ziara za kimasomo nchini South Korea, China akiwa na wanafunzi wenzake katika matamasha ya elimu na michezo. Baada ya kumaliza kidato cha nne, Happy alifanikiwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Strathclyde cha Uingereza ambapo anasomea digrii ya Biashara.
Happy aliwahi kuwa msichana pekee kutoka Tanzania aliyeweka historia ya kuongoza nchi zaidi ya 150 za mtandao wa IGCSE katika somo la Uhasibu kwenye mitihani ya kidato cha nne mwaka 2010.
Safari yake ya kushiriki katika mashindano ya urembo ilianzia kipindi alipokuwa likizo, baada ya kujikuta amekosa kitu cha kufanya ‘kuwa idle’ aliamua kushiriki Miss Dodoma 2013 na kufanikiwa kuibuka kuwa mshindi, na baadaye Miss kanda ya kati na hatimaye Miss Tanzania 2013.
Akiwa katika shindano la Miss Tanzania, Happy alikuwa ni mshiriki wa kwanza kuingia Nusu Fainali ya mashindano hayo kwa kutwaa taji la Redd’s Miss Photogenic 2013.