Majuto anasema kuwa ana watoto tisa
ingawa hakuwa tayari kuwazungumzia mama wa watoto hao zaidi ya
kumwongelea mkewe wa sasa, Aisha Mbwana kwa kuwa wake zake aliozaa nao
baadhi ya watoto kwa bahati mbaya walishafariki dunia.
Alisema kuwa yanapokuja masuala ya
familia huwa anapenda azungumze mkewe na kwa ridhaa yake. Kwa mujibu wa
Majuto anapenda aitwe mke halali kwa kuwa wake feki anao wengi kupitia
michezo ya kuigiza na wengine wenye fikira potofu hutumia picha hizo
kutengeneza habari za uongo.
Aisha anaizungumziaje familia yake
Kama kawaida ya wanawake wa Tanga ana
lafudhi ya huko ambayo huvutia kuzungumza nao, anaanza kwa kunieleza
kuwa alianza kuitwa mke halali wa nguli huyo wa sanaa za maigizo mwaka
1997, walipofunga ndoa .
Anasema kuwa alikutana na nguli huyo
maeneo ya Buguruni, Dar es Salaam, ambako alikuwa akiishi na dada yake
aliyekuwa kaolewa na rafiki yake mzee Majuto, ‘Mwanachia’ (kwa sasa ni
marehemu), ambaye walikuwa wakiigiza pamoja.
Anasema hakuwa na hili wala lile hadi
alipoamua kuondoka na kurudi kwao maeneo ya Vingunguti, ambako ndiko
walikokuwa wanaishi wazazi wake na kupewa taarifa kuwa posa imepelekwa
kwa ajili yake.
“Nilipoambiwa kuhusu hiyo posa
sikufikiria kama atakuwa ni mzee Majuto kwa kuwa alikuwa ni kama shemeji
yangu kutokana na kuwa karibu na shemeji yangu,” anasema Aisha ambaye
ni mama wa watoto watatu.
Anaendelea kueleza kuwa siku ambayo
wanafamilia walikutana na kumuuliza kama anamfahamu mchumba na kutajiwa
jina kuwa ni Amri Athumani, aliuliza mara mbili kwa kuwa alikuwa
hamfahamu huyo mtu hadi alipoambiwa kuwa ni King Majuto.
“Kwa mila za Wabondei mchumba wa kwanza
anakubaliana na wazazi, halafu binti anapewa taarifa na kwa kuwa wazazi
ni wakubwa inabidi binti akubali, na ndivyo ilivyokuwa kwangu nikakubali
na kuolewa na Majuto,” anasema mama huyo.
Anaingia kwenye uigizaji kufuata nyayo za mumewe
Aisha anafafanuwa kuwa kabla ya kuolewa
na Majuto hakuwa mwigizaji lakini baada ya kuolewa, mumewe huyo
alimwingiza kwenye uigizaji na filamu ya kwanza kuigiza na mumewe huyo
ni ‘Fukara hatabiriki’.
Mkewe huyo anasema kipindi hicho Majuto
alikuwa anafanya kazi bila kuwa na kikundi zaidi ya wanafamilia, hivyo
na yeye alikuwa mmoja wao akicheza kama mama na Majuto kama baba.