Mauaji ya kikatili yanayodaiwa
kufanywa na Kikundi cha Chinjachinja dhidi ya vikongwe, yamezidi
kuutikisa Mkoa wa Geita baada ya kikongwe mwingine, kuuawa kwa kukatwa
kwa mapanga akiwa nyumbani kwake.
Marehemu huyo ametajwa kuwa ni, Maua Ikoti(60) mkazi wa Kasang'hwa, wilayani Geita .
Mauaji hayo yamekuja huku takwimu
zikionyesha kuwa vikongwe watatu, wameuawa na kikundi hicho katika
kipindi cha wiki nne zilizopita.
Baadhi ya watu wanahusisha maujai hayo na imani za kishirikina.
Tukio la mauaji hayo lilitokea saa 6
usiku wa kuamkia juzi baada ya wauaji kuvamia familia hiyo na kisha
kuingia ndani ya chumba alimokuwa amekala kikongwe huyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha
Kasang'hwa, Maganiko Ndiomali, alisema wauaji walimkata kwa mapanga
kikongwe huyo kichwani,mikono na kwenye matiti.
Alisema pamoja na mayowe yaliyopigwa
na watoto wa marehemu ili kuomba msaada, juhudi za wananchi kuwasaka
wauaji hazikuzaa matunda.
Kuna madai kuwa kikundi
kinachohusishwa na mauaji hayo kimekuwa kikodiwa na baadhi ya watu ili
kulipiza kisasi baada ya kufiwa na ndugu zao wakiamini kwamba wamerogwa.
Kikundi hicho kinadaiwa kuhusika na
mauaji ya kikatili dhidi ya Mondesta Nchambi (53) mkazi wa kitongoji cha
Isabilo wilayani Chato kwa kumchinja mithili ya kuku.
Kamanda wa polisi mkoani
Geita,Leonard Paulo alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo lakini alisema
hadi sasa hakuna mtu au watu waliokamatwa wakihusishwa na mauaji hayo.
Source-Mwananchi