Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi
kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake
litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.
Jeshi la Polisi
limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na
baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile Kanuni za
Usalama Viwanjani za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA)
zinakataza silaha viwanjani.
Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika
upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu
Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba. Wote waliokutwa na silaha
hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki.
Hivyo, kwa washabiki
wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala
yake tunawashauri kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.
Pia
tunatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha
uwanja kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili
aweze kuchukuliwa hatua.